Kocha wa muda wa timu ya taifa ya Argentina, Lionel Scaloni amesema jezi namba kumi haitotumika katika kipindi hiki ambacho mshambuliaji na nahodha wa timu hiyo Lionel Messi ameomba kupumzishwa hadi mwakani.

Scaloni ametoa ufafanuzi huo akiwa katika mkutano na waandishi wa habari mjini New Jersey- Marekani, ulipokua unazungumzia pambano la kimataifa la kirafiki la Argentina dhidi ya Colombia litakaloshuhudiwa baadaye hii leo.

Kocha huyo amesema jezi namba kumi itaendelea kuheshimiwa na hawatoweza kumpa mchezaji mwingine kuitumia katika kipindi hiki, kutokana na muhusika kuomba udhuru kwa muda.

Amesema endapo Messi angetangaza kujiuzulu kuitumikia Argentina, jezi hiyo ingetumiwa na mchezaji mwingine yeyote katika kikosi cha sasa, lakini kuendelea kuwepo kwake kunaashiria kuwa namba hiyo bado ni halali kwa mshambuliaji huyo wa FC Barcelona.

“Namba ya jezi ni heshima kwa mchezaji anaeitumia katika kikosi, siwezi kusema ni halali kwa mtu mwingine kuitumia kwa sasa, kwa sababu muhusika bado yupo,” alisema. “Na alichokifanya ni kuomba udhuru wa kupumzika na baadae atarejea,” aliongeza.

“Tutakua tumekosea heshima na kumtenga, endapo jezi namba kumi itatumika katika kipindi hiki. Binafsi ninapenda kufanya mambo kiutaratibu na kwa kuwaheshimu wengine, ili kutoa nafasi kwa kila mmoja kujihisi ni sehemu ya timu hii,” alifafanua.

Messi alianza kukosekana katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki uliochezwa juma lililopita nchini Marekani, ambapo Argentina iliibuka na ushindi wa 3-0 dhidi ya Guatemala.

Bongo Star Search yarejea upya, Madam Rita atoa ombi Serikalini
Video: Waumini wa kanisa wanaokula majani kuwa karibu na Mungu

Comments

comments