Jeshi la Polisi Mkoani Kagera limejipanga kuimarisha ulinzi na usalama nyumbani kwao marehemu, Ruge Mutahaba ambaye alikuwa mkurugenzi wa uzalishaji wa vipindi Clouds Media Group atakapozikwa nyumbani kwao kijiji cha Kiziru Kata ya Karabagaine Jumatatu ya Machi 4 mwaka huu,
 
Hayo yamesemwa na Kamanda wa Polisi mkoa wa Kagera, Revocatus Malimi alipokuwa akizungumza na Dar24 Media ambapo amesema kuwa wataweka kambi katika eneo la msiba wakiwemo askari kitengo cha usalama barabarani kuongoza magari ya wanaoingia kwaajili ya maombolezo
 
Amesema kuwa askari wataelekeza viongozi mbalimbali sehemu za kuweka vyombo vya usafiri na kuvilinda ili kuweza kuwadhibiti vibaka.
 
“Penye mkusanyiko wa watu hapakosi wahalifu wanaoweza kuiba mizigo ya waombolezaji ama vipuli vya vyombo vya usafiri hivyo kazi yetu ni kulinda usalama wa raia na mali zao,” amesema kamanda Malimi
 
Kwa upande wake, Baba mdogo wa Ruge, Spetatus Mbeikya amesema kuwa maandalizi ya kupokea mwili wa marehemu yamekamilika baada ya kuundwa kwa kamati ya msiba itakayohusika na mapokezi ya wageni.
 
Hata hivyo, viongozi wa vyama vya siasa na madhehebu ya dini wamefika katika msiba huo Bukoba mkoani Kagera kwaajili ya kuhudhuria mazishi yanayotarajiwa kufanyika siku ya jumatatu.
CCM Njombe yaomba radhi kuhusu mauaji ya watoto
BASATA wamshushia Dudu Baya nyundo nyingine nzito

Comments

comments