Jarida la Ujerumani lililokuwa la kwanza kuripoti tuhuma za ubakaji dhidi ya Cristiano Ronaldo limetangaza msimamo wake kuwa halina wasiwasi na nyaraka muhimu zilizotumika kuandika habari hizo.

Kauli ya jarida hilo imetolewa muda mfupi baada ya mwanasheria wa Ronaldo kueleza Jumatano hii kuwa nyaraka zilizotumika katika habari hizo ni za kugushi.

“Tuna uhakika kwa asilimia mia moja kuwa nyaraka tulizotumia kutoka kwa vyanzo mbalimbali ni nyaraka halisi. Hatuna sababu yoyote ya kuamini kuwa nyaraka hizo hazikuwa halisi,” limesema jarida hilo la Der Spiegel.

“Kama ilivyo kawaida yetu kabla ya kuchapisha habari yoyote kwenye Der Spiegel, tunahakiki ukweli wa habari zetu ikiwa ni pamoja na mapitio ya kisheria,” limeongeza.

Katika chapisho lake, jarida la Der Spiegel limeeleza kuwa Ronaldo aliwahi kukiri kuwa mrembo huyo alisema ‘hapana, acha’ katika usiku wa tukio hilo na kwamba mchezaji huyo aliomba radhi baadaye. Maelezo ambayo yamepingwa vikali na upande wa Ronaldo.

Mwanasheria wa mchezaji huyo ameeleza kuwa wataliburuza mahakamani jarida hilo kwani ndilo la kwanza kuchapisha tuhuma hizo.

Mke wa Trump adai ni kati ya walionyanyaswa zaidi duniani
Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Oktoba 12, 2018