Mshambuliaji Jamie Vardy amesaini mkataba mpya na uongozi wa klabu ya Leicester City, ambao utaendelea kumuweka King Power Stadium hadi mwaka 2002.

Vardy mwenye umri wa miaka 31, amekamilisha hatua ya kusaini mkataba mpya na klabu hiyo aliyoiwezesha kutwaa ubingwa wa England msimu wa 2015/16, baada ya kufikia makubaliano na viongozi ambao walihitaji aendelee kubaki kwa kipindi kingine cha miaka minne.

Mshambuliaji huyo alijiunga na Leicester City mwaka 2012 akitokea Fleetwood Town, ameonekana kuwa muhimili mkubwa katika safu ya ushambuliaji klabuni hapo, na mpaka sasa ameshafunga mabao 88 katika michuano yote aliyocheza.

Aliwahi kuhusishwa na taarifa za kutaka kusajiliwa na Arsenal msimu wa 2016/17, lakini hakuwa tayari kuihama Leicester City, kwa kusema bado anaamini anaweza kupata mafanikio makubwa akiwa na klabu hiyo, inayoshiriki ligi kuu ya England.

Akizungumza mara baada ya kukamilisha taratibu za kusaini mkataba mpya, Vardy alisema: “Kila mmoja anajua ni vipi ninavyoipenda klabu hii, ninaamini hakuna klabu nyingine yenye ubora kama Leicester City, nimeamua kuendelea kuwa hapa kwa ajili ya kusaka mafanikio zaidi, baada ya kufanikiwa kuwa sehemu ya wachezaji waliounda kikosi kilichotwaa ubingwa msimu wa 2015/16.”

Mshambuliaji huyo anatarajiwa kuwa sehemu ya kikosi cha Leicester City ambacho baadae kitafungua pazia la ligi kuu ya soka nchini England msimu wa 2018/19 kwa kucheza dhidi ya Man Utd kwenye uwanja wa Old Trafford.

Mipango ya Pep Guardiola yavurugwa
Video: Mamia wamuaga Mzee Majuto, atonesha mioyo ya Watanzania