Mshambuliaji wa klabu ya Leicester City, Jamie Vardy na beki Harry Maguire huenda wakakosa mchezo wa ufunguzi wa ligi kuu ya soka nchini England msimu wa 2018/19 dhidi ya Man Utd utakaochezwa Agosti 10.

Meneja wa klabu hiyo iliyotwaa ubingwa wa England msimu wa 2015/16, Claude Puel amesema uwezekano wa wawili hao kukosa mchezo huo wa ufunguzi ni mkubwa kutoka na kuendelea kuwa na likizo ya mapumziko baada ya kumaliza jukumu la kuitumikia timu ya taifa kwenye Fainali za Kombe la Dunia na kushika nafasi ya nne.

Meneja huyo amesema mpaka sasa wawili hao hawajajumuika na wenzao katika maandalizi ya msimu mpya na endapo wataanza maandalizi hawatokua tayari kucheza mchezo huo ambao utachezwa kwenye uwanja wa Old Trafford.

“Kama tunajali afya zao na kufuata utaratibu hawatopaswa kucheza mchezo dhidi ya Man Utd, hawatokua na mazoezi ya kutosha, wataanza mazoezi siku tano kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa ligi,” alisema Pel.

“Hivyo hawatokua na muda wa kutosha kwenda sambamba na wenzao walioanza mazoezi kwa zaidi ya majuma mawili. Hatutaki kuwaharakisha. Ni wachezaji muhimu sana katika kikosi changu lakini linapokuja suala la kufuata utaratibu, tunapaswa kuheshimu na kuangalia hali zao kama binaadamu,” aliongeza.

Wakati Pael akithibitisha kutokua na uhakika wa kuwatumia wachezaji hao wawili, upande wa meneja wa Man Utd Jose Mourinho naye ana matumaini hafifu ya kuwatumia baadhi ya wachezaji wake, ambao walikua sehemu ya vikosi vya England, Ufaransa na Ubelgiji wakati wa fainali za kombe la dunia zilizomalizika Julai 15 nchini Urusi.

Katika maandalizi ya kuelekea msimu mpya wa ligi na mchezo huo wa ufunguzi dhidi ya Man Utd, kikosi cha Leicester City usiku wa kuamkia leo kilicheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Valencia CF ya Hispania na kulazimishwa sare ya bao moja kwa moja.

Mwishoni mwa juma hili kikosi cha Leicester City kitacheza mchezo wa mwisho wa kirafiki dhidi ya klabu ya Lille ya Ufaransa.

Bwege: Zitto hana makosa, makosa ninayo mimi
Rais wa Croatia aweka rekodi Kenya, atafutwa zaidi Julai