Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini imesema kuwa Baraza la Vyama vya Siasa linatarajiwa kukutana, tarehe 10 na 11 Januari, 2019 katika kikao cha kawaida cha Baraza hilo Michenzani mjini Unguja, Zanzibar.

Mkuu wa Sekretarieti ya Baraza la Vyama vya Siasa ambaye ni Msajili wa Vyama hivyo, Jaji Francis Mutungi na Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa. John Shibuda wameshauriana na kukubaliana kuwa, ni vyema kikao cha Baraza la Vyama vya Siasa kifanyike mapema.

Aidha, katika taarifa iliyotolewa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, imesema kuwa wameamua kufanya kikao hicho mapema ili kuwezesha Baraza kuandaa maoni yake kuhusu Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa na kuyawasilisha katika Kamati husika ya Bunge inayooanza shughuli zake tarehe 14 Januari, 2019.

Kikao cha Baraza la Vyama vya Siasa kitatanguliwa na Semina kwa wajumbe wa Baraza kuhusu utaratibu wa kutunga Sheria, itakayotolewa na Ofisi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika ofisi ndogo za Bunge Zanzibar zilizopo eneo la Tunguu.

Baadhi ya ajenda za kikao zitakazo jadiliwa ni pamoja na taarifa mbalimbali zinazohusu Baraza la Vyama vya Siasa, kujadili muswaada wa Sheria mpya ya Vyama vya Siasa na uchaguzi wa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Baraza.

Hawafiki popote na maazimio yao- Mrema
Emery ajutia kumkataa Salah, atamani kumsaini leo