Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo amewataka wazazi kutowasumbua watoto wao kwa kuwahamisha shule za serikali na kuwapeleka shule binafsi.

Ameyasema hayo jijini Dodoma alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, ambapo amesema kuwa shule za serikali zimefanya vizuri ikilinganishwa na ufaulu wa kipindi cha nyuma ambapo kila mtu alizibeza.

Amesema kuwa siri ya shule za serikali kufanya vizuri kwenye matokeo ya kidato cha sita mwaka 2019 ni kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa kwenye sekta ya elimu.

Aidha, amesema kuwa uwekezaji huo umepelekea ufaulu kupanda kutoka asilimia 98.2 hadi 98.93, huku shule nne za serikali kuingia katika kumi bora ya kwanza na katika shule 100 bora mwaka huu shule 64 ni za serikali ambazo 52 ni za kata na 12 ni shule kongwe na vipaji maalum.

Waziri Jafo pia amezitaja shule nne zilizoingia 10 bora kuwa ni Kisimiri, Mwandeti, Tabora boys na Kibaha.

Katika hatua nyingine Waziri Jafo ameipongeza mikoa mitatu ambayo ni Arusha, Tabora na Pwani ambazo shule za serikali zimefanya vizuri kwa kuingia 10 bora.

Hata hivyo, Waziri Jafo ameagiza kufanyika tathmini kwa mkoa wa Mara ambao takribani shule 3 zipo kwenye kundi la shule zilizofanya vibaya katika matokeo hayo.

 

IGP Sirro aonya kuhusu rushwa ndani ya jeshi la polisi
Prof. Mbarawa aanza kutekeleza agizo la JPM