Rapa Izzo Bizness amesema kuwa muziki wa kizazi kipya umekwama kwa sababu matukio ya aibu na yanayozua gumzo yamepewa nafasi kuliko ubora wa kazi inayofanyika.

Izzo amedai kuwa wasanii wa Tanzania kutotajwa kwenye orodha ya wanaowania tuzo za BET mwaka huu ni sehemu tu ya ishara ya kuporomoka katika maana ya muziki.

Rapa huyo amerusha makombora kwa baadhi ya vyombo vya habari kuwa vimekuwa chanzo cha kutoa nafasi kwa wasanii ambao wanafanya ‘kiki’ kuliko wale ambao wanafanya kazi zao vizuri.

“Watu ambao wamekuwa wanafanya vizuri kuanzia kwenye content (maudhui), production (utayarishaji) wamekuwa hawapewi nafasi,” Izzo aliiambia Ladha 3600 ya E-Fm.

“Leo hii mimi ninaweza kufanya tukio ambalo ni aibu kwa watu wengi lakini linaeweza kuwa ndio tukio kubwa na likawa ndio lina-trend kwa hicho kipindi, muziki wetu ndio umahamia katika sekta hizo,” aliongeza.

Alitoa mfano wa rapa AKA wa Afrika Kusini ambaye ametajwa kwenye tuzo hizo mwaka huu akiwa na mafanikio ya kuuza zaidi ya nakala milioni mbili (Double Platinum) ya albam yake mpya, akisema kilichofanya auze ni maudhui na sio ‘kiki’.

“Kwa Tanzania, inabidi tu ufanye tukio fulani kesho utrend (uzue gumzo) uitwe kwenye mahojiano na vipindi vikubwa, usifiwe ndio uulizwe kuhusu muziki wako,” alisema.

Mkali huyo wa ‘Ridhiwani’ pia alisema kitu kingine kinachokwamisha muziki wa Tanzania ni kukosa makampuni yaliyo kwenye mfumo rasmi wa kusambaza albam za wasanii. Alisema hii ndio sababu hadi leo ni vigumu kwa msanii kuuza nakala 1,000 nchini.

Tuzo za BET zitafanyika Juni 23 nchini Marekani.

Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Juni 17, 2019
Tyson Fury amchakaza Tom Schwarz, amtumia ujumbe Deontay Wilder