Makamu Mkuu wa Jeshi la Iran linalofahamika kama ‘Revolutionary Guards’, Hossein Salami amezionya Marekani na Israel kuwa taifa hilo litalipa kisasi kwa kile inachoamini nchi hizo zilishiriki  katika shambulizi la Jumamosi wakati wa gwaride la kijeshi jijini Ahvaz.

Salami amesema kuwa Marekani na Israel watarajie kisasi cha aina yake kutokana na shambulio hilo, lililosababisha vifo vya watu 25.

“Mmewahi kuona namna tunavyolipa kisasi… mtaona kwamba kisasi chetu kitawapiga na mtajuta kwa kile mlichofanya,” Salami anakaririwa katika hotuba yake iliyorushwa moja kwa moja wakati wa maombolezo ya tukio hilo.

Maelfu ya waombolezaji walifurika katika mitaa ya jiji hilo la Ahvaz, wengi wakiwa wanapiga kelele “kifo kwa Israel na Marekani.”

Majeneza ya wanajeshi 12 pamoja na raia 13 yaliyofunikwa bendera ya taifa hilo yalikuwa yamebebwa na waombolezaji.

Aidha, wengi walibeba picha ya mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka minne aliyeuawa kwenye tukio hilo.

Jumamosi iliyopita, makombora yalirushwa kwenye jiji hilo katika eneo ambalo watu walikuwa wamekusanyika kushuhudia gwaride la kijeshi la kumbukumbu ya vita kati ya taifa hilo na Iraq kati ya mwaka 1980-88.

Wahudhuriaji walitawanyika, watoto na wanawake walionekana kwenye picha za video wakiwa katika hali ya taharuki wakitafuta namna ya kujinusuru, na baadhi ya wanajeshi wakitoa msaada.

Hata hivyo, Marekani kupitia balozi wake wa Saudi Arabia, imekanusha vikali kuhusika na tukio hilo.

Babajide Ojo kurudi Afrika
Anthony Joshua alivyotolewa kijasho na Mrusi, ashinda kwa KO