Wananchi wa Kijiji cha Ikondo Kata ya Ikondo kilichopo Lupembe wilaya ya Njombe wametishia kugoma kushiriki katika shughuli za maendeleo mbele ya mkuu wa wilaya ya Njombe, Ruth Msafiri endapo hawatapewa ruhusa ya kuwaleta waganga wa kienyeji maarufu Kama ‘LambaLamba’ ili waweze kusafisha kijiji chao ambacho kinatajwa kutawaliwa na washirikina wengi.

Wamesema kuwa wamelazimika kususia kujitokeza katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kuwa usalama wa maisha yao umetoweka kijijini hapo kwa kuwa kumekuwa na kesi nyingi za wanawake kuingiliwa kingono kimazingara huku wengine wakijikuta wamelala wakiamkia chooni.

Wakizungumza katika mkutano wa hadhara mbele ya mkuu wa wilaya, wamesema kuwa serikali inatakiwa ione ulazima wa kuruhusu watalaamu hao wa Jadi kufika Kijijini hapo ili waweze kutokomeza ushirikina.

“Tunaomba mtusaidie tupo chini ya miguu yenu mkuu wa wilaya tunalia tunalala chooni, wakati wenzetu wa vijiji vya jirani wamepona kwanini sisi hapa tuzuiliwe? wenzenu msipotusaidia tutalala chooni, hakika tusipokubaliwa sisi hapa hatutafanya maendeleo kamwe nisema chonde mheshimiwa hili ulichukue,”wamesema wananchi hao

Kwa upande wake, mkuu wa wilaya ya Njombe, Ruth Msafiri amesema kuwa ujio wa watalaamu hao utahatarisha amani katika eneo hilo na kwamba endapo kama wanania njema ya kusafisha kijiji bila ya kusababisha machafuko waripoti ofisini kwake ili aweze kujiridhisha na uhalali wa vibali na vitambulisho vya kufanya kazi hiyo.

Naye, mwenyekiti wa kitongoji cha Idyadya na Diwani wa Kata ya Ikondo, Yohane Mhelela wamesema kuwa wananchi wamekuwa kikwazo cha ujio wa Lambalamba huku pia wakidai kuwa watalaamu hao wameharibu kabisa mfumo wa maendeleo kijijini hapo.

 

Lady Jay Dee akumbuka alivyomkimbilia Oliver Mtukudzi, alichopata
Wasiojulikana wazidi kutikisa mauaji ya watoto Njombe