Inspekta Jenerali wa Polisi Tanzania (IGP), Simon Sirro ameziagiza kampuni binafsi za ulinzi na wafanyakazi wa kampuni hizo kuhakikisha wamesajiliwa kwenye Mfumo wa  Kusimamia Sekta ya Ulinzi Binafsi (PSGP) hadi kufikia tarehe 31 Disemba 2020.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufanya kikao na wamiliki na wakurugenzi wa kampuni binafsi za ulinzi nchini kilichofanyika wiki iliyopita katika Ukumbi wa Bwalo la Maofisa wa Polisi (Police Officers Mess) uliopo Oyster Bay jijini Dar es Salaam; IGP Sirro alisema kuwa mfumo huo wa kusajili kampuni na wafanyakazi wake kwenye kanzi data maalum ndiyo njia ya kipekee ya kudhibiti changamoto katika sekta hiyo hususan askari wasio waaminifu.

IGP Sirro alisema kuwa mfumo huo ni mzuri na utaboresha sekta hiyo, lakini akasisitiza kuwa elimu zaidi inahitajika kwa wadau.

“Mfumo ni mzuri, lakini kitu kikubwa ni suala la elimu. Watu wakielimishwa nadhani wanaelewa, wakurugenzi wangu [wa makampuni binafsi ya ulinzi] wana elimu kubwa na wamekwenda shule wakipata elimu ya kutosha wataukubali mfumo,” alisema IGP Sirro.

“Kwa sababu askari leo anafanya uhalifu kwenye kampuni hii na anakwenda kwenye kampuni nyingine kufanya kazi, sasa bila kuwa na mfumo huu huwezi kumtambua huyu askari kwamba ni mbabaishaji,” aliongeza.

Aliwanyooshea kidole baadhi ya walinzi ambao huingia kwenye sekta hiyo wakiwa na lengo la kupeleleza njia zinazoweza kuwasaidia kufanya uhalifu na kwamba kupitia mfumo wa PSGP watadhibitiwa.

“Kuna baadhi ya askari hawa wa ulinzi binafsi anaingia kufanya kazi kwa lengo la wizi tu, anapelekwa kule anakuwa chambo kujua kinachofanyika ni kitu gani, lakini kwa kutumia mfumo [wa PSGP] ndiyo njia ya kipekee ya kuweza kudhibiti hili,” alifafanua.

IGP Sirro alisema kuwa amewaagiza wadau wa sekta hiyo ya ulinzi binafsi kukutana tena, kuhakikisha wanatatua dosari zilizopo ili wote kwa pamoja wakubaliane na mfumo huu.

Jeshi la polisi liliagiza kampuni zote binafsi za ulinzi pamoja na wafanyakazi wa kampuni hizo kuhakikisha wamesajiliwa kwenye PSGP kabla ya mwaka 2021 kwani baada ya Desemba 2020 wale ambao hawatakuwa wamesajiliwa kwenye mfumo huo hawataruhusiwa kufanya kazi kwenye sekta hiyo.

PSGP imeasisiwa na vyama vinavyosimamia sekta ya ulinzi binafsi, na kutekelezwa na Kampuni ya  Datavision International chini ya Usimamizi wa Jeshi la Polisi.  unaotumia teknolojia kuwasajili kwenye kanzi data kampuni pamoja na wafanyakazi wa kampuni binafsi za ulinzi, unasaidia upatikanaji wa taarifa za wadau hao kwa haraka ikiwa ni pamoja na kufahamu historia ya mlinzi husika, afya, tabia na mambo mengine.

Zaidi ya kampuni 174 na wafanyakazi 14,000 wamesajiliwa kwenye mfumo huo hadi kufikia siku ya kikao hicho na usajili unaendelea katika mikoa yote nchini.

Abdul Nondo atangaza kumrithi Zitto jimbo la Kigoma mjini

Mgumba abainisha mafanikio kwenye jimbo lake

Muigizaji nguli wa kike afariki kwa corona
Abdul Nondo atangaza kumrithi Zitto jimbo la Kigoma Mjini