Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro amesema kuwa wanafanya uchunguzi wa sauti zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii, zinazodaiwa ni za baadhi ya viongozi wa wastaafu wa Chama Cha Mapinduzi na Serikali.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na EATV/EARadio Digital, ambapo IGP Sirro amesema kuwa wameziona sauti hizo na wameanza kuzifanyia uchunguzi japo hajafahamu uchunguzi huo utakamilika baada ya muda gani na endapo itathibitika kuna makosa ya jinai, watuhumiwa watachukuliwa hatua za kisheria.

“Ni kweli hata sisi hizo sauti nimezisikia na tunafuatilia ili kujua ukweli wake, tukibaini kama kuna kesi ya jinai na kama yaliyokuwa yakitamkwa ni kweli basi tutachukua hatia za kisheria,” amesema Sirro

Wakati huohuo Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA kupitia msemaji wake, Semu Mwakyanjala, akizungumza katika kipindi cha East Africa Breakfast cha EA Radio, ameeleza kuwa suala hilo wamewaachia Jeshi la Polisi.

“Uhalifu wowote unaoripotiwa na TCRA watu wanaoshughulika na hilo ni Jeshi la Polisi, ila ninachosema kama kuna kosa la jinai, muhusika ashirikiane na Jeshi la Polisi ili ukweli ufahamike”, amesema Mwakyanjala.

Hata hivyo, hivi karibuni kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii, kulisambaa baadhi ya sauti zilizodaiwa kuwahusisha baadhi ya viongozi mbalimbali waliowahi kuwa ndani ya Serikali akiwemo Katibu Mkuu wa zamani wa CCM, Abdulrahmani Kinana, Waziri mstaafu wa Mambo ya Nje, Bernard Membe, Yusuph Makamba  na Nape Nnauye, zikizungumzia mambo mbalimbali ya serikali.

Video: Fahamu lishe bora kwa mtoto baada ya miezi 6
Video: UDUKUZI 'VITA' MPYA CCM, JPM awapa maagizo 11 Simbachawene, Bashe