Maandamano ya aina yoyote ni haki ya mwananchi na yanaruhusiwa kisheria lakini maandamano hayo lazima yafuate sheria na taratibu zilizobainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Sheria ya maandamano inamtaka mwananchi au kundi la wananchi wanaohitaji kufanya maandamano kutoa taarifa kwa maandishi kwa Mkuu wa Polisi wa eneo husika kabla ya masaa 48 ya kuanza kwa maandamano hayo ikieleza dhumuni la maandamano hayo.

Pia wahusika wanatakiwa wawe tayari kwa jibu lolote kutoka kwa mkuu huyo kwa kuwa chochote watakachojibiwa lazima kiwe na sababu.

Endapo wahusika watakataliwa kufanya maandamano na hawatoridhishwa na sababu zilizotolewa na Mkuu wa Polisi kuna hatua mbili muhimu zinazotakiwa kufuatwa na sio wahusika kujiamulia kuandamana kilazima kwa kuwa kufanya hivyo ni kosa.

Hatua hizo muhimu zinazotakiwa kufuatwa ni kuandika barua kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na kumueleza kutoridhishwa na sababu zilizotolewa na Mkuu wa Polisi ili Waziri naye kwa upande wake aamue kuruhusu au kukataza.

Endapo wahusika hawatoridhika na majibu ya Waziri, waandamanaji watatakiwa kwenda Mahakamani ambapo ndipo uamuzi wa mwisho utatolewa.

Hakuna sheria inayotambua maandamano ya nchi nzima kufanyika kwa siku moja kwa sababu kila eneo lina Mkuu wa Polisi mwenye haki ya kukubali au kukataa ombi la kufanya maandamano kulingana na hali halisi ya eneo lake.

Kila jambo lina faida na hasara zake lakini kuna mambo ambayo faida huwa chache kuliko hasara, maandamano yana athari kubwa kiuchumi na kijamii kwa sababu maandamano yoyote ni lazima Jeshi la Polisi liwajibike katika kuongoza na kulinda maandamano hayo, hivyo kupelekea wanajeshi wengi kusitisha kazi zingine kwa ajili ya kuzuia vurugu zisitokee.

Athari zingine ni kusitishwa kwa shughuli mbalimbali zikiwemo za usafiri , kufungwa kwa maduka na masoko pamoja na athari zitokanazo na vurugu zinazoweza kutokea kwa sababu ya maandamano hayo.

Hivyo itambulike kisheria hatia hizo zinatakiwa kufuatwa kabla ya kufanya maandamano, aidha maandamano kisheria ni jambo halali endapo tu litakuwa limehalalishwa kisheria.

Tweet ya Kikwete yazua gumzo mtandaoni
JPM aipongeza Wizara ya Ujenzi, awataka Chadema wakaandamane