Mchekeshaji Idris Sultan amemuomba msamaha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuhariri picha yake na kujiweka yeye.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Novemba 14, 2019 jijini Dar es Salaam, mchekeshaji huyo amesema kuwa ingawa hakuwa na nia mbaya anamuomba Rais amsamehe kama picha hiyo alimkwaza.

Mchekeshaji huyo ameeleza kuwa lengo la kuhariri picha hizo ilikuwa sehemu ya ubunifu wake kama msanii katika kumtakia Rais Magufuli heri ya kumbukizi ya siku yake ya kuzaliwa.

“Pamoja na nia yangu nzuri, na kwa bahati mbaya imetafsiriwa ndivyo sivyo, mimi kama binadamu nimeona nimuombe msamaha Rais mwenyewe kwa picha ile kama ilimkwaza,” alisema Sultan.

Sultan ambaye alishikiliwa na polisi kwa amri ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kutokana na kuweka mtandaoni picha aliyoihariri inayoonesha taswira yake akiwa amekaa kwenye kiti cha Rais John Magufuli, huku akiweka taswira ya Rais Magufuli kwenye picha yake akiwa amesimama na kuvalia suruali yenye mikanda inayopita mabegani, aliripoti mara tatu polisi pamoja na nyumba yake kupekuliwa.

“Kwa siku moja tukabadilishana kazi ili a-enjoy siku yake ya kuzaliwa kwa amani,” Idris aliandika kwenye picha hizo alizozihariri kwa kutumia teknolojia ya photoshop.

Kitendo hicho kilimuibua RC Makonda ambaye aliweka picha hizo kwenye Instagram na kuandika, “naona mipaka ya kazi yako hauijui nenda sasa hivi kituo chochote cha polisi uwaambie Makonda ameniambia nije, utakuta ujumbe wako.”

Agizo la Makonda lilizua mjadala mkubwa mtandaoni. Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla alijitokeza pia hadharani na kumtetea Sultan, akieleza kuwa anaamini Rais Magufuli hupenda utani na kwamba hatua hiyo haiwezi kuwa na nia ya kumuudhi. Dkt. Kigwangalla aliahidi kumtafutia Sultan mwanasheria.

Wakati sakata hilo halijafungwa rasmi, jana Idris Sultan aliweka Twitter picha nyingine akiwa amehariri jarada la kitabu kinachoelezea Maisha ya Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa na kuandika maneno yake.

Alipoulizwa leo na waandishi wa habari, alisema kuwa haoni kama kuna tatizo katika kufanya hivyo alieleza kuwa yeye haoni kama kuna tatizo.

Kei Kamara aiponda Sierra Leone
Wasio sajili laini kwa vidole kuendelea kupeta mwakani