Baada ya kutofanya vizuri kwenye mechi mbili zilizopita, Kocha Msaidizi wa Azam FC, Idd Cheche, ameweka wazi kuwa huu si wakati wa kuiondoa timu hiyo kwenye vita ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara (VPL).

Azam FC ambayo ni moja ya timu zilizo kwenye vita ya kuwania ubingwa huo msimu huu, katika mechi nne zilizopita za ligi imefanikiwa kuibuka na kushinda mchezo mmoja dhidi ya Ndanda (3-1), ikapoteza dhidi ya Yanga (2-1) na Simba (1-0) kabla ya jana kutoka sare ya ugenini na Kagera Sugar (1-1).

Matokeo hayo yameifanya Azam FC kufikisha jumla ya pointi 34 ikiwa nafasi ya tatu kwenye msimamo sawa na Yanga iliyonafasi ya pili kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa huku Simba ikiwa kileleni kwa pointi 41, zote mbili zikiwa na mchezo mmoja mkononi.

Akizungumza mara baada ya matokeo dhidi ya Kagera Sugar, Cheche alisema kuwa ligi bado inaendelea na lolote linaweza kutokea kwa timu hizo mbili za juu nazo kupoteza kama wao walivyopoteza.

“Sisi tunasema bado tunamechi nyingi kwa sababu kupoteza mechi moja au mbili sio kwamba kama mtu vile kuumwa, kuumwa siyo kufa, unaumwa unajiangalia nini tatizo unalifanyia kazi unajaribu kupambana.

“Kwa sababu mechi bado zinaendelea lolote linaweza kutokea kwa mtu mwingine kama sisi tumeweza kupoteza na mtu mwingine yoyote anaweza kupoteza kwa hiyo tunajipanga kwa ajili ya mchezo ujao (vs Lipuli) na mingine inaokuja tuhakikishe haturudii makosa,” alisema.

Alisema wanamshukuru mwenyezi Mungu kwa mchezo uliopita dhidi ya Kagera kuisha salama na kufanikiwa kuondoka na pointi moja ugenini mjini Bukoba huku akidai tatizo la safu ya ushambuliaji kushindwa kujiongeza limewaathiri hadi kupata matokeo hayo.

“Mchezo ulikuwa wa kiushindani ulikuwa mgumu, Kagera wanataka kushuka walikuwa wanataka kufa na mtu, wamepania, wamekuja kwa nguvu lakini na sisi kidogo watu wetu wamejituma kiasi ya uwezo wao lakini tulikuwa na kukosa kujiongeza kidogo hasa katika safu ya ushambuliaji, ambayo tulikuwa tunavitu kidogo tungejiongeza, tungeweza kushinda mchezo,” alisema.

Aelezea safu ya ulinzi

Akizungumzia kiufundi safu ya ulinzi kuruhusu bao kwenye kila mechi zote nne zilizopita za ligi, Cheche alisema safu hiyo imefanya kazi kubwa sana hadi sasa na kinachotokea ni sehemu ya mchezo.

“Beki yetu imejitahidi sana mua mrefu wamecheza kwa matokeo mazuri, lakini binadamu anakuwa binadamu hawezi kuwa na muendelezo kila siku vilevile, kuna siku anakuwa hakuamka vizuri au vipi, makosa madogo yametugharimu lakini kadiri siku zinavyokwenda tunazidi kufanyia kazi kuhakikisha hayajirudii tena,” alisema.

Cheche alimaliza kwa kuwaambia mashabiki wa Azam FC kuwa bado wanazidi kupambana kwa kila hali na mali kwa nguvu zote kuhakikisha wanarudisha heshima ile waliyokuwa nayo.

Tayari kikosi cha Azam FC kinadhaminiwa na Benki ya NMB, Maji safi ya Uhai Drinking Water na Tradegnts, kimesharejea jijini Dar es Salaam leo mchana kikitokea mjini Bukoba na ndege ya Shirika la Tanzania (ATCL), ambapo kesho Jumatano alfajiri kitaanza tena safari ya kuelekea mjini Iringa kucheza na Lipuli Ijumaa hii.

Alexandre Lacazette nje mwezi mmoja na nusu
Kyle Edmund ajitoa Argentina Open