Idadi ya wanajeshi wa Marekani waliojeruhiwa katika shambulizi la Iran kwenye makambi ya jeshi la nchi hiyo nchi Iraq imefikia 109, kwa mujibu wa taarifa rasmi za ‘White House’.

Majeruhi wametajwa kuathirika zaidi ubongo, madhara ambayo yameanza kuonekana kadiri siku zinavyoendelea. Iran ilitekeleza shambulizi hilo Januari 8 mwaka huu kulipa kisasi baada ya Marekani kumuua Kamanda wake, Qasem Soleimani.

Awali Rais Trump alisema hakuna aliyejeruhiwa kwenye tukio hilo, lakini baadaye Makao Makuu ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) walieleza kuwa wanajeshi 64 walijeruhiwa.

Pentagon waliongeza kuwa takribani asilimia 70 ya wanajeshi wake wamerejea kuendelea na kazi kwenye vituo vyao nchini Iraq.

Trump alieleza kuwa kutokana na kutokuwepo kwa majeruhi, ni sababu ya kutoishambulia Iran kama alivyokuwa ameahidi.

Mwezi jana, Trump alipoulizwa kuhusu uwepo wa majeruhi waliopata matatizo ya ubongo, alisema “nimesikia kuwa wana matatizo ya kuumwa kichwa na mambo mengine, lakini naweza kusema sio kwa kiasi kikubwa.”

Aliongeza kuwa hawezi kuichukulia kama ni majeraha makubwa kwa kulinganisha na majeraha amabayo amewahi kuyaona.

Kwa mujibu wa Serikali ya Marekani, zaidi ya askari 400,000 wametibiwa ugonjwa wa majeraha ya ubongo tangu mwaka 2000.

Corona yaathiri utalii nchini
Kitimoto inavyochangia ugonjwa wa kifafa