Pambano kati ya bingwa wa masumbwi duniani, Jeff Horn na Terrence Crawford lililoahirishwa hivi karibuni limepangwa kufanyika Juni 9 mwaka huu.

Pambano hilo ambalo ni moja kati ya mapambano yaliyokuwa yanasubiriwa kwa hamu na wapenzi wa ndondi, liliahirishwa baada ya Terrence kupata majeraha katika mkono wake wa kulia wakati wa mazoezi. Awali, pambano hilo lilikuwa limepangwa  kufanyika Aprili 14 mwaka huu.

Horn ambaye alimvua mkanda wa ubingwa bondia machachari, Manny Pacquiao katika pambano lililofanyika nchini Australia, atapigana kwa mara ya kwanza nchini Marekani ambako mchezo huo una wapenzi wengi na huingiza fedha nyingi zaidi.

Bondia huyo kutoka Australia analazimika kutetea ubingwa wake kwa mujibu wa taratibu za Shirikisho la Ngumi Duniani (WBO).

Hata hivyo, pambani hilo lililokuwa limepangwa kufanyika kwenye ukumbi wa Mandalay Bay Casino, Las Vegas limehamishiwa kwenye ukumbi wa MGM Grand Garden Arena ambapo Mei 2015 dunia ilishuhudia pambano la kihistoria kati ya Floyd Mayweather na Manny Pacquiao.

Wadau wa masumbwi wamekuwa na maoni mbalimbali juu ya pambano hilo kuhamishiwa katika ukumbi huo wakieleza kuwa kuyalinganisha mapamano hayo mawili ni sawa na kulinganisha wingi wa maji ya kwenye dimbwi na yaliyoko baharini.

Pambano la Mayweather na Pacquiao liliweka rekodi ya mapato ambayo haijawahi kuvunjwa.

Mbaroni kwa kubaka wakionesha ‘Live’ Facebook
Boko Haram wamng’ang’ania msichana mmoja kwa udini