Ndoto ya vijana 12 kati ya 325 ya waliochaguliwa kujiunga na mafunzo ya jeshi la kujenga taifa (JKT) mkoani mtwara, imezimwa baada ya kugundulika kuwa na ugonjwa wa homa ya ini na kuenguliwa katika kujiunga na mafunzo hayo.

Imeelezwa kuwa vijana hao wameenguliwa katika hatua za mwisho za kujiunga na jeshi hilo baada ya vipimo waliyofanyiwa kubainisha wana ungonjwa huo.

Taarifa hiyo imebainishwa na Mkuu wa mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa, wakati akifungua kikao cha kamati ya Ushauri ya mkoa jana, amesema vijana 12 kati ya 325 waliofanyiwa usaili kwa ajili ya kujiunga na JKT mkoani humo wamebainika wana homa ya ini.

Byakanwa amesema kuwa kati ya hao vijana 10 wanatoka wilaya ya Nanyumbu na wawili wanatoka wilaya ya Newala.

Hata hivyo Mkuu huyo wa mkoa amesikitishwa na taarifa ya vipimo hivyo kutoka kwa mganga Mkuu wa Mkoa kwa kuwa vijana hao tayari walikuwa katika hatua ya mwisho kujiunga na jeshi hilo, lakini kutokana na changamoto hiyo ya kiafya imebidi waenguliwe.

Huku tayari ameshatoa maagizo kwa mganga Mkuu wa Mkoa kuwachukua vijana hao na kuandaa utaratibu bora zaidi kuhakikisha wanapata matibabu sahihi ya ugonjwa huo.

“Hili siyo jambo la kufurahisha, vijana hawa kilichowatokea, kugundulika na homa ya ini” alisema Byakanwa.

Mganga Mkuu wa hospitali ya Mkoa wa Mtwara, Silvia Mamkwe, amesema homa ya ini ni ugonjwa ambao hushambulia ini na kusababisha ini kuvimba, huku akitaja baadhi ya sababu zinazopelekea mtu kupata ugonjwa huo zikiwemo sumu kuingia mwilini, matumizi ya pombe, maambukizI kutoka kwa mgonjwa na matumizi holela ya dawa.

“kuna aina tano za homa ya ini na mtu anaweza kupata maambukizI ya virusi hivi kwa sababu mbalimbali ikiwemo damu ya mgonjwa kugusana na damu ya mtu mwingine” aliongeza Silvia.

Aidha Mganga huyo ametaja baadhi ya dalili za awali za ugonjwa wa ini kuwa ni pamoja na uchovu, homa, kuharisha, maumivu ya tumbo na mwili kuwa na manjano.

 

 

Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Julai 21, 2019
Ushauri: Ni namna gani unaweza kuacha pombe