Daktari wa timu ya Chelsea, mwanadada Eva Carneiro wiki hii amepigwa stop kuendelea kukaa katika benchi la timu hiyo na mazoezini kwa ujumla, kutokana na kutokuelewana na meneja wa klabu hiyo Jose Mourinho.

Katika tukio lililotokea wikend iliyopita Chelsea wakitoa sare ya 2-2 na Swansea katika uwanja wa Stamford Bridge, Mourinho katika hali isiyo ya kawaida, alimbwatukia daktari huyo mwanamke kwa kile alichosema, daktari huyo alichelewesha muda wakati timu yao inahitaji matokeo kwa kwenda kumtibu Eden Hazard ambaye Mourinho anaamini hakuumia bali alikua kachoka.

Kauli hizi za Mourinho zimewashangaza wengi na kuwakera wengi wa mashabiki wa klabu hiyo kwa kumuona Mourinho amekosa busara na heshima mbele ya taaluma ya dada huyo aliyekaa klabuni hapo tangu mwaka 2009.

Penye wengi, pana mengi pia. Kupitia katika mitandao ya kijamii, mashabiki mbalimbali ulimwenguni kote waliandika hisia zao kutokana na sakata hilo.

Lakini kama ilivyo kawaida, penye wengi, wapo waliomtusi kocha wao Jose Mourinho, lakini hawakukosa waliomdhihaki mwanadada huyo kwa kuhusisha utendaji kazi wake na jinsia yake.

Juzi, daktari huyo aliandika kupitia ukurasa wake wa Facebook, kuwashukuru mashabiki duniani kote kwa meseji za faraja katika wakati huu mgumu kwake.

Eva, amefungiwa kukaa katika benchi wala kuhudhuria mazoezi ya timu yake na kocha Jose Mourinho raia wa Ureno, ingawa ataendelea wazifa wake wa kuwa daktari namba moja wa timu.

Wachambuzi wa mambo ya jinsia nchini England, wanahusisha tukio hili na lile lililokuwa kati ya kocha huyo huyo Mourinho walipozozana na mke wa kocha wa Real Madrid, Rafael Benitez wiki iliyopita, baada ya Jose Mourinho kumkashifu Benitez kuwa ana kitambi.

Katika ugomvi huo na mke wa Benitez, Mourinho alimtaka mwanamke huyo kuacha kuingilia mambo yasiyo muhusu na badala yake akamkashifu kwa kumtaka akae nyumbani na kumuandalia chakula mumewe.

Matukio haya yote mawili kati ya Mourinho na wanawake hawa yanaleta tafakari ya ubaguzi wa kijiinsia ‘sexism’ ambao Mourinho kauanzisha katika soka.

Kwa nini lakini haya yote? Mourinho anasema alikasirishwa na kitendo cha daktari huyo kuingia uwanjani kumtibia Eden Hazard kwa anachokiamini Mourinho kwamba Hazard alikua kachoka. Lakini mikanda ya kipande hicho yanaonesha kwamba daktari huyo aliitwa na mwamuzi akafanye kazi yake.

Wachambuzi wengi wanaamini Mourinho yuko katika wakati mgumu ‘stress’ kutokana na kutofanya usajili mzuri huku akitakiwa kutetea ubingwa wa ligi hiyo ya nchini England, sanjari na kufanya vizuri katika michuano mingine, huku timu yake ikionekana kutokuwa imara.

Makocha wengi wamekuwa wagumu kuweka ukweli hadharani na badala yake, wamekuwa wakitafuta mbuzi wa kumtoa kafara, ili upepo upite.

Pep Guadiola pia aliwatupia lawama, madaktari wa klabu yake ya Bayern Munich baada tu ya kula kichapo cha goli 3-1 mbele ya FC Porto ya Ureno katika michuano ya klabu bingwa ulaya mwaka jana.

Je, hali itakuwaje Stamford Bridge? Tusubiri kuona nini kitajiri siku za usoni. Je, utawala wa juu utayabariki maamuzi ya Mourinho dhidi ya daktari huyo? Na vipi timu, itapata matokeo mfululizo baada ya kuondolewa kwa daktari huyo katika benchi? Muda utasema.

Mke Wa H Baba Amzuia Kuichezea ‘Toto’
Euro 2016 Kumfukuzisha Hodgson