Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameziagiza kamati za ulinzi na usalama za mikoa na wilaya kuhakikisha zinachukua hatua kali dhidi ya watu wote watakaobainika wanaingiza nchini bidhaa za chakula na mafuta ya kupikia kwa njia za magendo.

Ametoa agizo hilo bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la mbunge wa Viti Maalumu, Zainab Vullu katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu ameziagiza mamlaka husika kuhakikisha zinaendelea kudhibiti uingizwaji holela wa bidhaa mbalimbali za vyakula visivyokuwa na virutubisho yakiwemo mafuta ya kupikia na kutoa adhabu kali kwa wafanyabiashara watakaobainika kuingiza bidhaa hizo nchini.

Aidha, mbunge huyo alihoji kuhusiana na suala la uagizwaji wa mafuta ya kupikia kutoka nje kama unazingatia sheria iliyopitishwa na Serikali ambayo inayolazimisha vyakula na mafuta ya kula kuwekwa virutubisho.

Akijibu swali hilo, Majaliwa amesema kuwa ipo sheria (Sheria ya chakula, Dawa na Vipodozi, Sura 219) inayohusu udhibiti wa vyakula yakiwemo mafuta ya kupikia ambayo inasimamiwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na imeweka utaratibu wa kudhibiti uzalishaji, uagizaji, usambazaji pamoja na uhifadhi wa mafuta.

“Sheria hiyo pia inataka vyakula vyote vikiwemo vile vilivyoagizwa kutoka nje ya nchi na vinavyozalishwa hapa nchini yakiwemo mafuta ya kupikia, lazima viwekewe virutubisho. Wafanyabiashara wanapaswa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa ili kulinda afya ya mlaji.”amesema Majaliwa

Hata hivyo, ameongeza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii inakusudia kuanzisha kurugenzi au idara itakayosimamia fukwe zote nchini zikiwemo za bahari na maziwa ili kuziimarisha na kuzifanya ziwe miongoni mwa vivutio vya utalii nchini.

 

 

Mtolea ajiunga rasmi na CCM
Tanzania yanyimwa msaada wa dola mil. 9 kisa kuzuia Ushoga