Serikali imesema hakuna kijiji nchini kitakachoachwa bila ya kuunganishiwa umeme katika awamu ya tatu ya mradi unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (Rea).

Hayo yamesemwa na Mbunge wa Jimbo la Vwawa Mkoani Songwe ambaye pia ni Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga wakati wa mikutano yake katika kijiji cha Igale na Iyula A vilivyopo katika kata ya Iyula akiwa katika ziara ya kikazi jimboni humo iliyoanza juzi tarehe 22 Octoba 2018.

Amesema kuwa serikali imetenga Sh1 trilioni kwa ajili ya kusambaza umeme katika vijiji 8,000 ambavyo bado havijaunganishiwa na nishati hiyo huku ikiendelea na uwekaji wa umeme katika vijiji zaidi ya 13400.

Hasunga amewahakikishia wananchi kuhusu upatikanaji wa umeme katika jimbo hilo hivyo wananchi wanapaswa kuondoa wasiwasi na serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli.

Amesema kuwa utekelezaji wa miradi hiyo ya umeme katika Jimbo la Vwawa unaenda sambamba na lengo la Serikali ya awamu ya Tano ya kuwa na uchumi wa kati kupitia viwanda ifikapo 2025.

Aidha, Hasunga amewataka wananchi hao kutumia fursa mbalimbali zitakazotokana na utekelezaji wa miradi katika sekta ya gesi na mafuta ili kujiongezea kipato na kuiwezesha nchi kutimiza malengo yake kuelekea kuwa nchi ya uchumi wa kati.

Kuhusu malalamiko ya wananchi dhidi ya gharama kubwa za pembejeo za kilimo, Mhe Hasunga ambaye ni Waziri wa Kilimo amewahakikishia wananchi kuwa wizara yake imejipanga kuhakikisha kuwa mbolea zinapatikana kwa wakati ili wakulima wa mazao mbalimbali ya chakula na biashara waweze kunufaika na pembejeo hizo.

Amesema kuwa kumekuwa na malalamiko mengi nay a muda mrefu kuhusu mbolea hivyo serikali itapitia upya utaratibu wa uuzaji wa mbolea ili kutafuta namna bora ya kurahisisha huduma hiyo kwa wakulima nchini.

Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Desemba 27, 2018
Maaskofu wapigilia msumari vita ya ushoga, CCM yawaangukia marafiki wa Lowassa