Harmonize amesimulia jinsi alivyopigiwa simu majira ya saa kumi usiku na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli baada ya kuangalia video ya wimbo wake ‘Magufuli’ ambao aliubadili kutoka kwenye wimbo aliomshirikisha Diamond Platinumz ‘Kwangwaru’.

Ameiambia XXL ya Clouds FM kuwa ulikuwa usiku wa aina yake kwake baada ya kupokea simu na kusikia sauti ya Rais Magufuli.

”Aliwahi kunipigia simu ilikuwa saa kumi usiku akaniamabia nashukuru sana wimbo wako unajenga nchi, maendeleo yapo lakini kuna wengine wapo vijijini hawajui kama Dar es Salaam kuna airport (uwanja wa ndege) au hata kuna mwendokasi lakini kupitia wimbo wako umeonesha kila kitu,” amesema Harmonize.

Ameongeza kuwa baadaye Rais Magufuli alimpa Mama Janeth ambaye alimuelezea kuwa ndiye shabiki wake mkubwa na alimsalimia.

Akizungumzia kauli ya Rais kuwa angependa awe Mbunge wa Tandahimba, Harmonize amesema kuwa kauli ya Rais ni amri hivyo hawezi kuikataa. Hivyo, amesema yeye na wananchi wa Tandahimba watakaa waone jinsi ya kuitekeleza. Jimbo la Tandahimba hivi sasa liko chini ya Mbunge anayetoka chama cha Wananchi (CUF),  Katani Ahmed.

Amesema baada ya kauli hiyo ya Rais Magufuli amekuwa akiangaliwa kwa mtazamo tofauti hata na makampuni ambayo yanataka kumpa kazi.

Leo, Harmonize ameachia wimbo wake mpya wa kwanza akiwa rasmi nje ya kundi la WCB alioupa jina la ‘Uno’. Wimbo wa mwisho ulikuwa ‘Inabana’ aliomshirikisha Kenzo kutoka Uganda lakini wimbo huo ulikuwa na lebo ya WCB hata kwenye video yake ya YouTube hali inayoonesha kuwa iko chini ya menejimenti hiyo.

Mtoto achomwa viganja na wazazi kisa kupoteza simu
Harmonize: Niliuza nyumba kuwalipa WCB Sh Milioni 500, sikuruhusiwa kutumia nyimbo