Halmashauri ya Wilaya ya Njombe mkoani Njombe, imetoa Mikopo kwa Vikundi 86 vya wanawake, Vijana na watu wenye ulemavu yenye thamani ya Fedha za Kitanzania kiasi cha milioni 194 ikiwa ni Utekelezaji wa agizo la Serikali.

Mikopo hiyo ilitolewa kwa Awamu mbili tofauti, Awamu ya kwanza Mwezi February 2019, Halmashauri hiyo ilitoa mikopo yenye thamani ya Tsh. milioni 66 katika vikundi 36, na Awamu ya Pili ilitolewa mikopo yenye thamani ya Tsh. Milioni 128 katika vikundi 50 vilivyopo kwenye Kata tofauti tofauti za Halmashauri hiyo.

Akisoma taarifa ya mikopo ya awamu ya pili, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Ally Juma Ally amesema kuwa kwa mwaka 2018/2019 halmashauri hiyo imeviwezesha vikundi 59 vya wanawake, Vijana vikundi 22 na watu wenye ulemavu vikundi vitano.

Aidha, Mkurugenzi huyo amebainisha kuwa kati ya Shilingi Milioni 194 zilizokopeshwa, Milioni 143 ni mchango wa mapato ya ndani ya halmashauri, Shilingi Milioni 51 zinatokana na marejesho ya Mikopo ya awali na kuongeza kuwa Halmashauri hiyo imevuka lengo kwa kutoa mikopo kwa asilimia 135 kati ya asilimia 100 zilizowekewa malengo kwa mwaka 2018/2019.

Kwa Upande wake Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Ruth Msafiri ambaye alikuwa mgeni rasmi katika makabidhiano ya mikopo hiyo amewataka wanufaika wa mikopo hiyo kuitumia ipasavyo katika kujikwamua kiuchumi pamoja na kuirejesha kwa wakati ili Serikali kupitia halmashauri ya Njombe iendelee kutoa mikopo mingine kwa wahitaji.

Baadhi ya Wanufaika wa mikopo hiyo wakiwemo watu wenye ulemavu wameipongeza halmashauri ya Wilaya ya Njombe kwa kutambua umuhimu wa Vikundi vyao na kuvisaidi kupata Fedha ili waweze kuendesha shughuli zao za Ujasiriamali kwa lengo la kujikwamua kiuchumi.

Mwalimu mkuu atuhumiwa kumpa mimba mwanafunzi wake
Nguvu ya pesa ipo, lakini mkono wa Mungu hauepukiki- Makonda