Maafisa wa Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) nchini Kenya, wamemkamata Hakimu  Mkuu wa Mahakama ya Mombasa, Edgar Kagoni baada ya kilo 10 za dawa za kulevya aina ya Heroin zilizokuwa katika chumba cha ushahidi kupotea.

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini humo aliwaambia waandishi wa habari Ijumaa iliyopita kuwa madawa hayo ya kulevya yalikuwa na thamani ya Sh.30 Milioni za Kenya na yalipotea pamoja na fedha taslimu Sh. 600,000 za Kenya.

Alisema kuwa wanamshikilia Hakimu Kagoni pamoja na watu wengine watatu na wamewafungulia mashtaka kwa makosa ya kutaka kupoteza haki na kusaidia biashara ya dawa za kulevya.

Mwendesha Mashtaka wa Serikali naye alitoa ufafanuzi kuhusu mashtaka yanayomkabili hakimu huyo.

“Kiasi hicho cha kielelezo cha ushahidi ambacho ni madawa ya kulevya na fedha vilipotea katika chumba cha kutunzia ushahidi kati ya Juni 28, 2019 na Julai 26, 2019,” taarifa ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali imeeleza.

Taarifa hiyo imeeleza pia kuwa Hakimu Kagoni ndiye aliyemfunga mtuhumiwa wa dawa hizo za kulevya, Hussein Massoud Eid kifungo cha miaka 30 jela, Juni 11, 2019.

Hakimu huyo pia alimpiga faini ya Sh. Milioni 90, mtuhumiwa huyo baada ya kukutwa na hatia ya kuhusika na biashara ya dawa hizo za kulevya.

Namna ya kujitibu maumivu ya korodani nyumbani
Trump afuta mazungumzo na kundi la Taliban, amlilia mwanajeshi wake