Taasisi za tiba na afya katika nchi mbalimbali duniani zimejifungia zikijaribu kutengeneza dawa ya virusi vipya ya corona (covid-19), lakini gharama za utengenezaji wa dawa ya aina yoyote na muda utakaotumika hadi kuithibitisha huenda ikawa kikwazo kwa baadhi ya taasisi.

Dkt. Bernhards Ogutu wa Kenya Medical Research Institute (KEMRI) amekaririwa na vyombo vya habari nchini humo akieleza kuwa utengenezaji wa dawa unaweza kugharimu zaidi ya $1 bilioni, na kwamba huchukua angalau miaka saba ikiwa inajaribiwa kabla ya kupata uthibitisho rasmi na kuanza kuuzwa.

Dkt. Ogutu ni mbombezi wa dawa na tiba ambaye amehusika katika kutengeneza dawa mbalimbali ikiwa ni pamoja na dawa ya kinga dhidi ya malaria; ambayo imeanza kutumika kwa awamu kwa watoto katika nchi nane duniani kote.

Serikali ya Kenya iliithinisha matumizi ya dawa hiyo iliyotengenezwa kwa msaada wa mashirika mbalimbali ya nje.

Ameeleza kuwa kuandaa dawa ya tiba ni mchakato mrefu ambao nchi chache zinaweza kuumudu bila kutegemea msaada. Alizitaja nchi za Afrika zinazoweza kufanya uendelezaji wa dawa kwa teknolojia waliyonayo ni Afrika Kusini, Senegal, Misri, Morocco na Ethiopia.

Alisema uandaaji wa dawa kuanzia hatua ya kwanza kwa kawaida unaweza kuchukua hadi miaka 7 kama dawa hiyo haitengenezwi kwa kuchanganya dawa zilizopo na ni gharama kubwa sana.

“Ni mchakato mrefu sana na ni kazi nzito,” alisema Dkt. Ogutu. Aliongeza, “na bila kushirikiana taasisi, Serikali na wadau uendelezaji wa dawa tu kupata dawa mpya kwa ajili ya ugonjwa uliopo hautawezekana.”

Wanasayansi wa Kenya wameshahusishwa katika utafiti wa taarifa za dawa mbalimbali duniani. Kwa mujibu wa Dkt. Ogutu, kadiri wanavyozidi kushiriki wamekuwa wakipokea maombi zaidi ya kufanya mapitio ya taarifa za dawa ambazo ziko kwenye kipindi cha majaribio.

Juzi, Rais Kenyatta aliliambia Taifa hilo kuwa wataalam wa tiba kutoka Kenya wanaungana na juhudi za dunia nzima katika kutafuta dawa ya covid-19.

Tangu mwaka 1990, wanasayansi wa Kenya kupitia KEMRI wameshafanya mapitio ya dawa zilizohusika kwa ajili ya Ebola, VVU/Ukimwi, Polio, Pneumonia na kufanya majaribio kwa baadhi ya watu waliojitolea.

Hivi karibuni, Marekani imeishutumu China kwa madai kuwa inajaribu kuiibia taarifa za utafiti wake wa dawa ya covid-19, na kwamba wamejaribu kufanya udukuzi kwenye taasisi zake za afya.

Marekani inaamini kuwa hakuna kitu chenye thamani kubwa zaidi hivi sasa duniani kama dawa ya covid-19, na kwamba atakayekuwa wa kwanza kuibaini na ikathibitishwa na Shirika la Afya Duniani atakuwa amepata heshima ya kihistoria mbali na faida za kibiashara.

Kilomoni aibuka, ahoji nguvu ya wanachama Simba SC

Serikali yaingilia kati hatma Maghorofa yaliojaa maji Mbweni

Tshishimbi awapa matumaini Young Africans
Azam FC: Simba SC waje mezani