Gari la wagonjwa (ambulance) la mkoa wa Mara limekamatwa likiwa linasafirisha kilo 800 za mirungi huku likiwa linapiga ving’ora kama limebeba mgonjwa.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima, gari hilo lenye namba za usajili DFPA 2955 linalomilikiwa na Halmashauri ya Mji wa Tarime, lilikamatwa katika wilaya ya Bunda saa chache baada ya dereva wa gari hilo  kukataa kumfuata mgonjwa kutoka wilaya ya Tarime kumpeleka Hospiali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza.

Mkuu huyo wa mkoa amesema kuwa awali, dereva wa gari hilo, George Matai alidai kuwa ana udhuru wa kifamilia na kwamba gari hilo halina mafuta. Hivyo, mgonjwa huyo alisafirishwa kwa gari la jeshi la polisi.

Lakini walipokuwa wanapita wilayani Bunda, waliliona gari hilo na ndipo askari walipoamua kulifuata na kulikagua. Alisema kufuatia ukaguzi huo walibaini limesheheni madawa ya kulevya aina ya mirungi.

“Mambo kama haya ndiyo yanayotupaka tope Mkoa wa Mara na tunaonekana wa hovyo sana,” alisema Malima. “Mwananchi anakosa huduma huku rasilimali zikituika kwenye mambo ya kipuuzi kama haya. Hili halivumiliki kamwe lazima hatua kali za kisheria zichukuliwe,” aliongeza.

Jeshi la polisi mkoani humo limemkamata dereva na watu kadhaa ambao wanadaiwa kuwa ni mtandao uliosuka na kufanya biashara hiyo, kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Juma Ndaki.

Kamanda Ndaki alisema kuwa mirungi hiyo ilikuwa inapelekwa jijini Mwanza kwa wakala ambaye hakumtaja jina. Aliongeza kuwa  dereva alikuwa anapiga ving’ora kwa lengo la kuwarubuni askari wa usalama barabarani wasiwasimamishe kwa kudhani kuwa amebeba mgonjwa.

Video: COSTECH yatoa ufafanuzi kuhusu barua iliyosambaa juu ya Twaweza
Jeshi la Hamisa lampa tabu Ray C, amshambulia ‘wewe ni sumu’