Meneja wa klabu ya Chelsea Frank Lampard amepanga kuwashangaza Arsenal kwa kupeleka ofa ya kumsajili mshambuliaji wao Pierre-Emerick Aubameyang wakati dirisha la uhamisho wa majira ya kiangazi litakapofunguliwa.

Aubameyang ambaye pia ni nahodha wa kikosi cha The Gunners, anamaliza mkataba 2021, huku ripoti zikidai kwamba mshambuliaji huyo wa kimataifa kutoka Gabon anaweza kuruhusiwa kuondoka kama itawekwa mezani ada inayozidi Pauni milioni 20.

Meneja wa Arsenal Mikel Arteta anataka kumbakiza Aubameyang kwa muda mrefu, lakini mabosi wake hawapo tayari kuona wanashindwa kupata pesa kwa kumuuza na kumwaacha aondoke bure mwakani.

Arsenal waliumizwa kwa kumshuhudia Aaron Ramsey akiondoka bure mwaka jana mkataba wake ulipokwisha na sasa watapata hasara nyingine ya Aubameyang kwa sababu watalazimika kumuuza kwenye dirisha lijalo la majira ya kiangazi huku thamani za wachezaji zikiwa zimeshuka kutokana na mtikisiko wa uchumi uliosababishwa na janga la corona.

Kwa mujibu wa Telegraph, Chelsea wanamtaka mshambuliaji huyo licha ya kufahamu kwamba haitakuwa kazi rahisi kwa Arsenal kuwakubalia wamchukue Aubameyang kutokana na upinzani uliopo baina yao.

Hata hivyo, dili hilo litafanyika kama tu The Blues watakwama kwenye chaguo lao la kwanza la kumnasa Timo Werner, ambaye anapewa kipaumbele na kocha Frank Lampard kwenda kuboresha safu yake ya ushambuliaji ambayo mwisho wa msimu itampoteza Willian.

Ruhsa mabadiliko ya wachezaji watano EPL
Corona yaibamiza Tottenham Hotspur