Familia za marehemu Steven Kanumba na Amri Athuman maarufu kwa jina la King Majuto zimelipwa Shilingi milioni 45 baada ya kamati ya kupitia mikataba ya wadau wa filamu iliyoundwa na Serikali kufanya kazi ya kupitia upya mikataba ya wasanii.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe leo Aprili 18, 2019 wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2019/2020.

“Baadhi ya kampuni zimethibitisha kuwalipa wahusika viwango vya kuridhisha na nyingine zimeingia kwenye makubaliano maalum na kamati ya kuongeza viwango mbalimbali,” amesema.

Kufuatia tangazo la wizara kupitia upya mikataba mibovu waliyoingia baadhi ya wasanii na hivyo kuathiri kipato chao, kamati ya kupitia mikataba ya wadau wa filamu iliundwa na kuchambua mikataba 11 iliyowasilishwa.

Waziri Mwakyembe ametoa mfano kampuni za Pan Afrika Enterprises Ltd na Ivori Iringa zimeingiza kwenye akaunti maalum Sh 30 milioni kwa kazi alizotekeleza marehemu King Majuto kimkataba.

“Azam-SSB imeandaa malipo ya ziada ya Sh 20 milioni na kampuni ya Tanform ya Arusha Sh 15milioni ambayo yatawasilishwa kwa msimamizi wa miradhi ya marehemu King Majuto,” amesema.

Pia amesema kuwa baadhi ya kampuni ikiwamo Neelkanth Salt Ltd zimejiwekea utaratibu wa kuridhisha wa mawasiliano ya moja kwa moja na familia ya King Majuto.

Amesema kampuni ya Steps Entertainment imemkabidhi mama wa marehemu Steven Kanumba ziada ya Sh 15 milioni na kwamba kampuni hiyo imeahidi kushirikiana naye kuandaa filamu ya maisha ya mwanawe.

Zaidi ya miezi 10 iliyopita Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe aliunda kamati ya wanasheria kwa lengo la kupitia upya mikataba ya wasanii ili waweze kulipwa fidia zao kwani wasanii wamekuwa wakifanya kazi kubwa na makampuni mbalimbali bila kunufaika kutoka kwa makampuni hayo.

Mwakyembe alisema kwa kuanzaa ameunda kamati maalumu ya wanasheria kukagua mikataba yote ya mashirika na makampuni waliyoingia wasanii King Majuto na marehemu Seteven Kanumba ‘Kanumba’ na endapo kutakuwa na uonevu wowote watalipwa fidia.

Mwakyembe alifikia hatua hiyo baada ya msanii wa filamu na mchekeshaji maarufu nchini, Amri Athuman maarufu King Majuto (ambaye ameshatangulia mbele za haki) akiomba msaada wa Shilingi laki tano (500,000) kwa ajili ya matibabu huku kuna makampuni yaliyofaidika naye kwa kuingia mikataba na kufanya naye baadhi ya matangazo ambayo mpaka sasa yanarushwa katika vyombo mbalimbali vya habari na makampuni hayo kuendelea kunufaika.

Rais ajiua kukwepa mikono ya polisi
Rais Magufuli atoa wiki moja kwa Wizara ya Ardhi, Wizara ya Viwanda kumpatia mwekezaji eneo