Mahakama ya wilaya ya Mpwapwa imewahukumu watu watatu akiwemo baba na mwanae wakazi wa kijiji cha Msagali darajani kata ya Chunyu wilayani Mpwapwa kila mmoja kifungo cha miaka 30Jela baada ya kupatikana na hatia ya unyang’anyi wa kutumia silaha.

Watu hao ni Baba mzazi Raphael Mkwai wa miaka (54) na mwanae Kombozo Kenneth( 30) pamoja na shemeji wa baba huyo, Msafiri Machimo (22) wenye kesi namba 130 ya mwaka 2017 iliyokuwa inasikilizwa na Hakimu mkazi wa mahakama ya wilaya hiyo, Pascal Mayumba na mwendesha mashitaka wa polisi Stephen Masawa.

Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Mayumba ameiambia mahakama kuwa watuhumiwa wote watatu siku ya tarehe 27. 12. 2017 Katika kijiji cha Msagali darajani walimshambulia, Charles Mponi kwa kumkatakata na vitu vyenye ncha Kali sehemu mbalimbali za mwili wake na kumsababishia majeraha mwilini mwake ikiwemo kichwani mikoni na miguuni na kupora kiasi cha shilingi milioni moja na simu.

Aidha Hakimu Mayumba amesema bila halali  watuhumiwa walitenda kosa hilo kinyume na sheria namba 287(A)namba 16 ya kanuni ya adhabu., ambapo amesema kuwa mashahidi nane wa kesi walijitokeza hivyo mahakama ilijiridhisha na kutoa hukumu hiyo.

Katika utetezi wao mtuhumiwa namba moja na namba mbili walisema hawana la kusema hivyo wanamuachia Mungu, huku mtuhumiwa namba tatu akiomba mahakama iwapunguzie adhabu kwa kuwa familia nzima watakuwa gerezani na kuwaacha watoto wao bila kuwa na uangalizi wa karibu.

Ikumbukwe awali watuhumiwa wawili Raphael Mkwai na Kombozo Kenneth walihukumiwa miaka 8 Jela kabla hajapatikana mtuhumiwa namba 3 ambae alikuwa ni Msafiri Machimo aliye kamatwa Tanga akiwa na simu ya Mhanga.

Kwa upande wake mwendesha mashitaka wa polisi, Stephen Masawa ameiomba mahakama itoe adhabu kali kwa watuhumiwa kutokana na madhara makubwa aliyoyapata mhanga huku akiwaasa vijana kupenda kujishughulisha na kuachana na kujihusisha na uhalifu.

Hata hivyo, hakimu Mayumba ameambia mahakama kuwa watuhumiwa hao watafungwa kifungo cha miaka 30 kila mmoja Jela kutokana na kupatikana na hatia na kutokana na ushahidi na vielelezo vilivyo wasilishwa mahakanani lakini akatoa nafasi ya kukata rufaa kwa yule ambaye atakuwa hajaridhika na hukumu hiyo.

 

Majaliwa amkaanga Mkurugenzi wilaya ya Rombo, 'Nakupa siku 16'
EWURA kuanzisha vituo vya mafuta vinavyotembea

Comments

comments