Uongozi wa klabu ya Inter Milan umeonyesha kuwa tayari kufanya mazungumzo na FC Barcelona, ambao wameonyesha nia ya kumsajili mshambuliaji kutoka Argentina Lautaro Martinez, wakati wa usajili wa majira ya kiangazi (Mwishoni mwa msimu huu).

Mpango wa usajili wa mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 22, umeanza kuteka vyombo mbalimbali vya habari barani Ulaya, kufuatia uwezo aliouonyesha msimu huu wa 2019/20 katika ligi ya Italia.

Kwa mujibu wa tovuti ya Tuttosport: Uongozi wa Inter Milan umetangaza dau la Euro milioni 150 kama ada ya uhamisho wa Martinez sambamba na kiungo wa Brazil na klabu ya Barcelona ya Hispania Arthur Henrique Ramos de Oliveira Melo, kama sehemu ya dili hilo.

Hata hivyo inahisiwa huenda FC Barcelona wakaomba kupunguziwa kiasi hicho cha pesa, ambacho kinadhaniwa huenda kikawa kikubwa kwa mabingwa hao wa Hispania.

Kabla ya kumtaja Arthur Melo kama sehemu ya dili la uhamisho wa Martinez, Inter Milan walianza kumpendekeza Arturo Vidal ama Ivan Rakitic, lakini baadae walibadili msimamo wa kuelekeza nguvu kwa mbrazil huyo.

Arthur amekua kwenye wakati mgumu wa kupata nafasi katika kikosi cha kwanza cha FC Barcelona, kufuatia majeraha ya muda mrefu yaliyokua yakimkabili.

Kiungo huyo ambaye alisajiliwa na FC Barcelona msimu uliopita akitokea Grêmio kwa dau la Euro milioni 31, amecheza michezo 12 kwa msimu huu wa 2019/20.

CORONA: Mtibwa Sugar waondoka Tanga
Video: Maduka na masoko hayajafungwa - PM