Waimbaji kutoka Uganda ambao ni ndugu wa tumbo moja, Esther mwenye umri wa miaka 14  na Ezekiel Mutesasira mwenye umri wa miaka 11, usiku wa kuamkia leo wametangazwa kuwa washindi wa shindano la vipaji la ‘East Africa’s Got Talent’ na kupewa $50,000 milioni (sawa na Sh 115 milioni za Tanzania).

Waimbaji hao ambao ni watoto wa Mchungaji Steven Mutesasira, mwanzilishi wa Kanisa la Anointed Upper Room, walikuwa miongoni mwa makundi ya washiriki sita waliofanikiwa kuingia katika fainali za mashindano hayo jana usiku, ukiwa ni msimu wa kwanza ulioandika historia kwa mara ya kwanza mashindano hayo kufanyika Afrika Mashariki.

Watoto hao wamethibitisha angalau uhalisia wa msemo maarufu wa Kiswahili, ‘mtoto wa nyoka ni nyoka’, kwakuwa baba yao na mama yao ni waimbaji wazuri wa nyimbo za injili.

Wengine walioingia fainali ni DNA, Spelicast, mtoto Janell Tamara, Jehova Shallom, Intayoberana. Wote walileta ushindani mkali lakini kura za watazamaji zilikuwa nyingi zaidi kwa ndugu hao, Esther na Ezekiel.

Mashindano hayo yaliyofanyika jijini Nairobi nchini Kenya, yaliongozwa na majaji Vanessa Mdee kutoka Tanzania, Jeff Koinange kutoka Kenya, Gaetano Kongwa kutoka Uganda na Makenda kutoka Rwanda.

Mshereheshaji wa mashindano hayo, Kansiime aliibua shangwe baada ya kuwatangaza watoto hao kuwa washindi na kukamilisha safari ya miezi sita ya msimu wa kwanza wa East Africa’s Got Talent.

Video: JPM amtumbua kigogo polisi juu kwa juu, Panya buku usipime
Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Oktoba 7, 2019