Wanasema siasa ni mchezo mchafu, lakini mimi naamini siasa ni mchezo wenye mbinu (technique) kali zaidi ya ndondi ambazo uso wako ndio target ya adui yako wakati wote.

Wanasiasa wakongwe wanafahamu mbinu nyingi zaidi ya wanasiasa wapya, lakini wanasiasa wapya wanazifahamu vizuri zaidi mbinu mpya kuliko wanasiasa wakongwe. Hali hii imezua ushindani mkubwa katika ulingo wa siasa uliojaa wanasiasa wakongwe na wanasiasa wapya machachari.

Miongoni mwa wanasiasa hao wapya na machachali ni mbunge wa viti maalum aliyekuwa kada wa CCM na sasa ni Kamanda wa Chadema, Ester Bulaya mwenye umri wa miaka 35.

Ester ambaye ni mbunge wa viti maalum ameonesha uwezo mkubwa na mbinu mpya katika ulingo wa siasa hasa alipokuwa bungeni na katika eneo la Bunda Mkoani Mara, hali iliyomuwezesha kuaminika na kukubalika zaidi na wananchi wengi.

Bulaya alianza kuonesha umahiri katika ulimwengu wa siasa kwa kurusha masumbwi ya hoja alipokuwa bungeni huku akihoji masuala mazito na kuwatikisa baadhi ya mawaziri wa chama chake cha zamani bila kujali itikadi.

“Fedha ambazo ziko kwenye mfuko maalum, hazitakiwi kutumika kwa matumizi mengine kwa mujibu wa sheria. Kwa mujibu wa katiba, waziri umevunja Katiba, ibara ya 135 na ibara ya 136,” haya ni baadhi ya maneno ya Bulaya ndani ya Bunge akimueleza Waziri wa Fedha, Saada Mkuya.

Mbinu zake hazikuishia katikati ya nchi (Dodoma), aligundua kuwa hata ukipika chakula kitamu kiasi gani jikoni, hakitakuwa na maana kama hautakipakua kwa wahusika wakionje au wakile.

Hivyo, alifanya kila jitihada za kusaidia vijana na wananchi wengine mjini Bunda kutengeneza imani kwa wananchi kwa vitendo kama kutoa vifaa vya michezo kwa vijana ikiwa ni pamoja na kuanzisha na kuratibu Kombe la mpira wa miguu lililopewa jina lake.

Kasi ya Bulaya ilimshtua usingizini mbunge wa Jimbo la Bunda na waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira. Tetesi za kuwa Bulaya anataka kumpokonya Wasira tonge la Ubunge ziliongezeka kwa kasi.

Hivyo, wanasiasa hao wakaanza kuwa washindani wakubwa na mahasimu kisiasa. Kuna wakati Wasira alishindwa kuvumilia na kumrushia ‘neno’ Bulaya akidai kuwa yeye sio Mbunge wa Bunda bali anajipendekeza kwa majukumu yasiyomhusu.
wasira

Kulianza kupambazuka na ulingo wa siasa kuwaka moto wa pambano kali kati ya Stephen Wasira aliyetumikia serikali katika awamu zote nne na Ester Bulaya ambaye ni chipukizi machachari mwenye mbinu mpya. Wasira alianza kuona huyu sio mtoto baada ya kukutana na mayowe ya kuzomewa siku moja akiwa jimboni kwake Bunda. Waliozomea walidaiwa kuwa waamini wa sera za Bulaya.

Wakati CCM ikiwa inasubiri kura za maoni katika nafasi za ubunge, bila shaka Stephen Wasira ambaye kutokana na ukali wake kwenye siasa aliwahi kupewa jina la ‘Tyson’ alipokuwa chama cha upinzani, atakuwa alishapanga jinsi ya kumpiga ‘knock out’ Ester Bulaya kwa kutumia uzoefu wake ndani ya chama hicho na mbinu nyingine ili asivuke mstari huo.

Bulaya na gloves

Hata hivyo, kuzingatia uzito wa masumbwi ya ‘Tyson’, Ester Bulaya, pamoja na sababu nyingine nyingi aliona kutega uso ni kukaribisha kifo cha ndoto yake ya kuwa mbunge wa Bunda, na kukimbia si uoga bali ni sehemu ya mbinu ya mchezo ili kujipanga upya.

Juni 22, Ester Bulaya alipokelewa rasmi Chadema baada ya kutangaza kuitosa CCM. Mpango wake ni ule-ule kupanda ulingoni na Stephen Wasira lakini akiwa na ‘gloves’ za rangi za chama tofauti na kile cha kijani. Kwa nguvu alizopata akiwa na Chadema, kwa mara ya kwanza Ester alipaza sauti kutangaza vita ya kumg’oa Stephen Wasira katika nafasi ya ubunge bila kujali uzoefu.

“Makongoro Nyerere alisema, awamu ya kwanza upo, awamu ya pili upo, ya tatu upo ya nne upo, ya tano… mwisho wako umefika sasa,” alitamba Bulaya huku akipokelewa na sauti za nguvu za wafuasi wa Chadema, “Kamtoe Wasira”.

Sasa mwanasiasa huyo mwenye taaluma ya uandishi wa habari anatarajia kupambana na Stephen Wasira kugombea mkanda wa ubunge wa jimbo la Bunda.

Hata hivyo, Wasira ambaye alivua jina la utani la ‘Tyson’ bungeni mwanzoni mwa mwaka 2010 akisisitiza kuwa ni Rais wa Tanzania pekee mwenye ruhusa ya kumuita jina hilo, anatakiwa kuivuka ngazi ya kura za maoni kabla ya kukutana na Ester Bulaya.

Mzizi wa fitna na mbwembwe zote mwisho Oktoba 25 ambapo wananchi wa jimbo la Bunda wataungana na wananchi wa majimbo mengine nchini kuamua nani akawawakilishe bungeni na nani awe rais mpya wa Tanzania. Cha muhimu ni kujiandikisha ili uwe mmoja kati ya waamuzi hao.

CCM: Tume Ya Uchaguzi Imetudhalilisha
Mbowe Azungumzia Mgombea Urais Ukawa