Mkurugenzi wa michezo wa FC Barcelona Eric Abidal ataendelea na majukumu yake klabuni hapo kama kawaida, licha ya kuibuka majibizano kati yake na nahodha Lionel Messi, kufuatia sakata la kutimuliwa kwa meneja Ernesto Valverde.

Messi alimjibu kiongozi huyo juzi jumanne, kufuatia kauli iliyotolewa na Abidal, alipohojiwa na gazeti la Diario Sport kuhusu kiwango cha kikosi cha Barcelona, wakati wa utawala wa meneja Valverde.

Kiongozi huyo alidai wachezaji walikua wakicheza chini ya kiwango chini ya meneja huyo kutoka Hispania, jambo ambalo lilitoa msukumo wa kutangazwa kuondolewa kwenye majukumu ya ukuu wa benchi la ufundi la nafasi yake kuchukuliwa na Quique Setien mwezi uliopita.

Katika taarifa iliyotolewa kwenye gazeti la Diario Sport Abidal alinukuliwa akisema: “Wachezaji wengi walionyesha kubweteka na kujikuta wakicheza chini ya kiwango, jambo ambalo lilidhihirisha mapungufu mengi kwenye kikosi chetu.”

“Mahusiano ya meneja na wachezaji yalionekana kutokua mazuri, kufuatia kilichojidhihirisha uwanjani. Nililazimika kuushauri uongozi kutafuta mbinu mbadala ambazo zingeweza kuisaidia timu, na ndipo maamuzi ya kutimuliwa kwa Valverde yalipoanza kuchukua mkondo wake.”

Lakini Messi ambaye mwishoni mwa mwaka jana alifikisha idadi ya tuzo sita za mchezaji bora wa dunia (Ballon d’Or) alimjibu kwa kusema: “Nazungumza kutoka moyoni, sijapendezwa na jambo hili, ni bora mtu akajali nafasi yake kwa kusema ukweli na sio kuzungumza eti kwa sababu unaongeza na chombo cha habari kilichotaka kufahamu nini tatizo lililopelekea kuondoka kwa meneja aliyepita.”

“Wachezaji wanafahamu majukumu yao wanapokua uwanjani, na ndio maana kila mchezo tumekua tunajitahidi na kutoka uwanjani tukiwa na matokeo mazuri, ni mara chache sana inatokea tunapoteza, lakini bado kiwango kinaonekana kuvutia.”

Kufuatia majibizano hayo, uongozi wa FC Barcelona ulifanya kikao cha dharura na Abidal jana jumatano, na ilihisiwa egenda kubwa ilikua sakata lake na Messi kupitia vyombo vya habari.

Kikao hicho kilichukua zaidi ya saa mbili, lakini baadae uongozi wa Barcelona ukatangaza kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 40, ataendelea na majukumu yake kama kawaida.

Kauli ya Abidal, ambaye alicheza sambamba na Lionel Messi kuanzia mwaka 2007 hadi 2013, ilichukuliwa kama dharau kwa wachezaji wa FC Barcelona ambao waliiweka klabu hiyo katika nafasi ya nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa ligi ya Hispania (La Liga), kabla ya kutimuliwa kwa meneja Valverde.

Kwa sasa FC Barcelona inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi kwa kufikisha alama 46, ikitanguliwa na klabu ya Real Madrid inayomiliki alama 49.

Waziri Mkuu amjibu Mbowe, ''Vyama vya siasa havijazuiwa kufanya shughuli zake''
Membe alivyowasili kwenye Kamati ya CCM kuhojiwa