Karibu tena kwenye ‘Throwback Thursday (TBT)’, Alhamisi ya kumbukizi ya matukio yaliyojili, yakavuma na kuacha alama enzi hizo za Wahenga. Dar24 inakujuza ili tuendelee kufahamu tunakotoka, kutafakari tulipo na kukaza mwendo tuendako.

Mzazi wa Muziki wa Bongo Fleva, Dully Sykes, Bwana Misifa kama anavyopenda kufahamika ni moja kati ya wasanii ambao walikuwa na nguvu kubwa miaka takribani kumi iliyopita.

Uwezo wake na sauti yake adimu ilikuwa dhahabu kwenye muziki, hali iliyomlazimu mtayarishaji mahiri Master Jay kuhangaika kuhakikisha anainasa sauti hiyo ili kuukamilisha wimbo wa ‘Dhahabu’ uliokuwa umewakutanisha pia kwa mara ya kwanza Mr. Blue na Joslin. Ngoma hiyo ilikuwa moja kati ya kali zilizounda albam ya ‘Pamoja Ndani ya Game’ iliyotayarishwa na kumilikiwa na Master Jay.

Master Jay anaeleza kuwa baada ya kuweka ‘miadi’ na Dully ili afike studio kurekodi chorus na kibwagizo, ujio wake ulikuwa wa aina yake kwani alifika akiwa na msafara wa magari mazuri manne pamoja na wasichana wazuri ambao aliingia nao hadi kwenye chumba cha kuingizia sauti (booth).

“Dully alikuwa Dully, kipindi hicho… kwanza aliingia na convoy (msafara) wa magari kama manne na wapambe, akaja na watoto wakali nakumbuka watoto wanne, halafu yeye mwenyewe walikuwa ananukia zile pafyum hata mimi nilikuwa siwezi kumudu gharama,” Master Jay anasimulia kwenye XXL wiki hii.

Ameeleza kuwa Dully alipoingia tu studio alimpa dakika 20 kukamilisha kazi yake ili aendelee na mizunguko yake huku akiangalia saa kama bilionea mwenye mambo lukuki. Lakini mbwembwe za ‘Mr. Misifa’ hazikuishia hapo, alipoingia kwenye chumba cha kurekodia bado aliendelea kumuacha hoi Master Jay.

“Mic anatakiwa kuiangalia ikiwa mbele yake, lakini alikuwa anaangalia huku nyuma kwa sababu alikuwa yuko bize na wale watoto. Sasa namwambia tayari… basi anaimba huku anaangalia hivii(nyuma),” anaendelea kusimulia.

Hata hivyo, mbali na kuwa na mambo mengi ndani ya chumba cha kuingizia sauti, kazi aliyoifanya Dully iliacha alama kubwa na kuufanya wimbo huo kuwa mkubwa katikati ya nyimbo kubwa za ‘Pamoja Ndani ya Game’.

“Nilipata mafanikio makubwa sana kwenye ile albam. Na hata yeye mwenyewe naamini alipata mafanikio, lakini nilimrekodi kwenye mazingira magumu sana… pafyum, warembo kwenye vocal booth (chumba cha kuingizia sauti),” anasema Master Jay.

“Nakupenda Ma.. basi njoo maa. Ni kila saa kabisa kwako kichaa/Girl just listen tuishi kama heave, nakweka kwenye top ten, nadata na reception…” Dully Sykes alifungua mlango kwenye Dhahabu.

Hiyo ndio ilikuwa albam ya mwisho kwa Master Jay, baada ya hapo akaamua kustaafu kazi ya utayarishaji akiwaachia akina Macochali.

Uwezo mkubwa wa kuimba alionao Dully Sykes ambaye alianza kusikika zaidi kwa kurap kwenye ngoma kama Julieta na Nyambizi, na kisha kuwa mzazi wa mtindo wa ‘Mwanasesele’ ambao una mchango kwenye hii Bongo Fleva ya leo, ndio sababu kuu inayomfanya abaki kileleni katikati ya damu changa zinazofanya vizuri hadi leo.

Dully mwenyewe hupenda kusema “hii Bongo Fleva mimi nimeizaa.” Kwa waliozaliwa miaka 20 iliyopita inaweza kuwa ngumu kumuelewa, lakini neno hilo lina chembe nyingi za ukweli kwa wahenga walioiona Bongo Fleva ya waimbaji ilivyoanza.

Kwa leo tukumbuke hii, tukutane tena Alhamisi ijayo kwenye ‘TBT’.

Video: Fahamu nyoka hatari wenye sumu kali zaidi duniani
Video: Siku ya kurudi Lissu hii hapa, Kimbunga Mali za mabilioni zataifishwa

Comments

comments