Serikali imesema ipo katika mpango mkakati wa kurahisisha huduma za afya kwa wananchi ikiwemo kutumia ndege isiyo na rubani maarufu kama drone ili kusaidia kufikisha dawa kwa haraka kwa wagonjwa.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Josephat Kandege kwenye mkutano wa Kongamano la Wadau wa Mnyororo wa Ugavi wa Dawa- Tanzania (Tanzania Health Supply Chain Summit 2018) linalotarajiwa kufanyika kwa siku mbili jijini Dar es Salaam.

Kandege amesema dunia kila kukicha inabadilika hivyo waliopo ndani ya dunia ni lazima wakubaliane na mabadidiliko hayo na kuyakabili katika hali chanya hivyo Serikali ipo katika mpango mkakati wa kuwarahisishia huduma za afya wananchi wake.

”Katika uhalisia dunia inabadilika kwa kasi kubwa sana, huko tunakoenda tunategemea mwanachi ifike mahali kwamba hata dawa mtu anapelekewa kwa drone, upo nyumbani kwako tuweze kufanya vipimo kwa mwananchi lakini pia na dawa ziweze kumfuata mwananchi huko huko aliko” amesema Kandege.

Aidha amempongeza MSD kwa kazi ngumu na nzuri anayoifanya kwani kwa kiasi kikubwa kilio cha kutokuwepo kwa dawa hospitalini kimepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na mfumo wa uendeshaji mambo kubadilika kulinganisha na hali ilivyokuwa hapo awali amabpo fedha za dawa zilikuwa zinafikia Serikali za mitaa kwanza.

”Lazima nimpongeze MSD kwa kazi anayoifanya ukitazama siku za nyuma fedha inayoletwa lazima ipelekwe serikali za mitaa, ukienda kwenye zahanati unaambiwa hakuna dawa lakini fedha zipo halmashauri husika, lakini kwa utaratibu uliopo sasa dawa zinapelekwa moja kwa moja hadi zahanati hata kile kilio kilichokuwepo juu ya dawa sasa kimepungua” ameongezea Kandege.

Ameongezea kuwa ”Lazima tukubaliane dunia imekuwa kijiji na lazima tukubalianae na mabadiliko ya kiteknolojia, hivyo ni vyema kwenda na mabadiliko hayo”.

31 wafa poromoko la matope
Video: Hakuna kifo kibaya kama kifo cha moto na maji, hizi ni 'beach' hatarishi duniani