Mshambuliaji Zlatan Ibrahimovic huenda akarejea nchini Italia kujiunga na klabu ya AC Milan, baada ya kukamilisha mkataba wa kuitumikia klabu ya LA Galaxy, inayoshiriki ligi kuu ya soka Marekani MLS.

Kamishna wa ligi ya MLS Don Garber, ameweka wazi mpango huo, kwa kusema anaamini Ibrahimovic ana nafasi kubwa ya kuendelea kucheza soka la ushindani, na siku zote amekua akitamani kurejea kwenye ligi ya Italia (Serie A).

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 38, tayari ameshakamilisha jukumu la kuitumikia LA Galaxy kwa kipindi cha miezi 18 kwa mujibu wa mkataba wake, na hatosaini mkataba mpya.

Klabu ya AC Milan imekua katika harakati kubwa za kuhakikisha inampata mshambuliaji huyo raia wa Sweden, ili kuongeza chachu ya ushindani kwenye safu yake ya ushambuliaji.

Ibrahimovic aliwahi kuitumikia AC Milan kuanzia mwaka 2010 hadi 2012, na alifanikiwa kufunga mabao 42 katika michezo 61 ya ligi ya Italia (Serie A).

“Zlatan amekua katika mawindo makali ya AC Milan, na mara kadhaa amekua akiizungumzia klabu hiyo ambayo amekiri kuipenda katika kipindi chake chote alichocheza soka, ninaamini atakubali kujiunga nayo kwa mara nyingine tena,” alisema Garber alipohojiwa na ESPN.

“Kwa sasa ana umri wa miaka 38, ninaamini bado ana uwezo mkubwa wa kucheza soka la ushindani, na ndio maana AC Milan wamekua katika harakati za kuihitaji huduma yake.”

Ibrahamovic amewahi kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa ligi ya nchini Marekani (MLS Best XI) mara mbili mfululizo mwaka 2018 na 2019, kufuatia kufunga mabao 53.

Kwa bahati mbaya Ibrahamovic amemaliza msimu wa ligi ya Marekani kwa kushuhudia kikosi klabu yake ikikubali kichapo cha mabao matano kwa matatu dhidi ya Los Angeles Football Club, katika mchezo wa hatua ya nusu fainali kanda ya magharibi, mwezi uliopita.

Arsene Wenger: Sijaomba kazi FC Bayern Munich
Vyama vya ushirika vyakosa ubunifu utatuzi kero za wakulima