Hatimaye mchakato wa kumpata mgombea mmoja atakayepeperusha bendera ya Chama Cha Cha Mapinduzi (CCM) kwenye mbio za Urais Oktoba mwaka huu, umefika kileleni ambapo John Pombe Magufuli amechaguliwa kwa kura za kishindo na Mkutano Mkuu wa Taifa.

Matokeo yaliyowekwa kwenye akaunti ya twitter ya Chama hicho ambayo imekuwa ikitangulia kutoa matokeo hayo kabla ya kutangazwa rasmi na kuthibitika kuwa ya kweli baadae, yameonesha kuwa Magufuli ameshinda kwa kishindo cha asilimia 87 za kura zote zilizopigwa na wajumbe takribani 2480 kutoka mikoa yote ya Tanzania.

Magufuli amewashinda wagombea wenzake wawili walioingia kwenye hatua ya mwisho ya mchakato huo ambao ni Balozi Amina Ali aliyepata asilimia 10 ya kura zote na Dr. Asha Rose Migiro aliyepata asilimia 3 ya kura zote.

Mchakato huo ulianza kwa Kamati Kuu kuyachuja majina 38 yaliyowasilishwa na kuyapata majina ya January Makamba, Bernard Member, Dr. John Magufuli, Dr. Rose Migoro na Balozi Amina Ali. Majina hayo yalipelekwa kwenye Halmashauri Kuu ya chama hicho ambapo yalichujwa na kupatikana majina matatu wakiwaacha January Makamba na Bernard Membe.

Shangwe na nderemo zimeendelea kurindima katika ukumbi mpya wa Chama hicho ambapo wajumbe wameonekana kuwa na furaha kuu muda wote.

Hata hivyo, matokeo rasmi yanatarajiwa kutangazwa na viongozi wa chama hicho muda wowote kutoka katika Mkutano Mkuu wa Taifa unaoendelea mjini Dodoma.

Matokeo Rasmi: CCM Yampa Magufuli Ridhaa kwa kishindo
Wajumbe Wagomea Kikao Wakimtaka Lowassa, Kikwete Asema 'Haijawahi Kutokea'