Naibu Spika Dkt. Tulia Ackson amewatembelea na kuwapa pole baadhi ya Wananchi waliokumbwa na mafuriko katika kata ya Isyesye jijini Mbeya yaliyosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali kwenye mkoa huo huku baadhi ya watu wakilazimika kuyahama makazi yao kutokana na maji kujaa ndani ya nyumba.

Licha ya kuwapa pole waathirika wa mafuriko katika eneo hilo amebainisha kuwa serikali ipo katika juhudi za kuyaondoa maji katika makazi yao na kuwasihi wanapoanza ujenzi kuhakikisha yanaachwa maeneo ya maji kupita hasa nyakati za mvua.

”Nimekuja kuwapa pole ndugu zangu baada ya kupata taarifa za matatizo mliyoyapata lakini mfahamu ya kuwa Serikali ipo pamoja nanyi, hivi sasa inafanyika jitihada ya kuyaondoa haya maji lakini hata sisi wenyewe tushauriane tunapojenga nyumba zetu tuweze kutenga maeneo kwa ajili ya kuruhusu maji kupita” Amesema Dkt. Tulia

Aidha amewataka wananchi wa eneo hilo kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya kuenea kwa virusi vya Covid – 19 hasa kwa kukumbuka kunawa mikono mara kwa mara.

”Ndugu zangu mmesikia wito wa Rais na Serikali kuhusu hili janga la corona, hivyo tuliepuke kwa kutoshikana mikono lakini pia kila wakati tukumbuke kunawa mikono kwahiyo niwaombe sana kutilia maanani maagizo tunayopewa na viongozi wetu” . Amesema Dkt. Tulia.

Jinsi manjano yanavyotoa michirizi na mikunjo katika mwili
Corona: Watalii Tanzania watakiwa kusogeza mbele safari