Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson amesema kuwa anampango wa kugombea Ubunge katika uchaguzi mkuu wa 2020, lakini hajabainisha atagombea jimbo gani, kwa kile alichodai kuwa chama chake cha CCM, kinamzuia kutaja jimbo atakalogombea.

Ameyasema hayo wakati akizungumza kwenye kipindi cha East Africa BreakFast cha East Africa Radio, wakati akijibu swali la juu ya kuonekana kuonyesha nia ya kugombea Ubunge, kwenye jimbo la Mbeya Mjini.

Amesema kuwa Mwenyezi Mungu akijaalia uhai 2020 atagombea lakini hajataja ni jimbo gani, hivyo amewataka wananchi na wafuasi wake kuwa watulivu kwasasa, lakini muda ukifika ataweka wazi jimbo atakalogombea.

“Mwenyezi Mungu akitupa Uhai 2020 nitagombea, ila nitagombea wapi? naomba watulie kwa sababu chama chetu kina utaratibu wake ila nashukuru ninavyoonekana nina uwezo wa kugombea maeneo mengi.” amesema Tulia Ackson.

Aidha, amesema kuwa pale Mbeya Mjini kuna ofisi ya Tulia Trust, kwa hiyo wananchi wakisikia amefanya maendeleo maeneo mengine, pale Mbeya maombi yanakuwa ni mengi, lakini kuhusu watu kufikiri kwamba anataka Jimbo hilo, hawezi kusema.

Hata hivyo, Naibu Spika, Tulia Ackson ni miongoni mwa wadau wakubwa ambao wamejitokeza kuunga mkono shughuli mbalimbali za maendeleo katika jamii ya Watanzania.

MSD kujenga kituo cha mauzo na usambazaji dawa Simiyu
Zitto Kabwe bado ahitajika Polisi