Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, amekutana na kufanya mazungumzo na Binti wa Mfalme wa Jordan, Sarah Zeid ambaye ni Mwanaharakati wa masuala ya lishe, wanawake na watoto Duniani, jijini Dodoma.

Katika mazungumzo yao, Dkt. Mpango, amemweleza Princess Sarah Zeid kwamba Tanzania bado inakabiliwa na changamoto ya masuala ya lishe, utapiamlo na udumavu wa watoto licha ya nchi kuwa na chakula cha kutosha.

Amesema kuwa iwapo eneo la lishe halitasimamiwa kikamilifu Taifa litazalisha watoto wenye udumavu wa ubongo na kusababisha kupungua kwa uwezo wa kufikiri na utendaji hafifu wakiwa katika shughuli mbalimbali.

Ameitaja mikoa ambayo inazalisha mazao mengi kama Mbeya na Njombe lakini ina kiwango kikubwa cha watoto wenye utapiamlo, na kutoa wito kwa kila mtanzania kuhakikisha anaangalia ni chakula gani kinahitajika kwa ajili ya lishe ya watoto na wakinamama wajawazito ili kupunguza udumavu na vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga.

Aidha, amempongeza Mwana wa Mfalme wa Jordan, Sarah Zeid, kwa kampeni yake anayoifanya duniani kote kupambana na vifo vya wakinamama wajawazito na watoto kwa kuwa mchango wa wanawake ni mkubwa katika jamii ikiwemo uzalishaji mali.

“Nimeziagiza Wizara, Mikoa na Halmashauri zote nchini kutumia fungu lililotengwa kwa ajili ya lishe kwa matumizi yaliyopangwa ili kuhakikisha watanzania wanaimarika kiafya na kushiriki kikamilifu katika Shughuli za Maendeleo” Amesema Dkt. Mpango.

Kwa upande wake Mwana wa Mfalme wa Jordan, Sarah Zeid ambaye ameambatana na Mwakilishi wa Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) nchini Tanzania, Michael Dunford ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa jitihada zake katika kupambana na utapiamlo unaosababishwa na ukosefu wa lishe.

Naye Mwakilishi wa Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa-WFP nchini Tanzania, Michael Dunford amesema kuwa shirika lake linatambua mchango mkubwa wa Serikali katika kupambana na masuala ya lishe duni na shirika lake litaendelea kushirikiana nayo ili kufikia malengo yanayotarajiwa.

Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Machi 31, 2019
JPM awatunuku kamisheni maafisa 146 wa JWTZ