Waziri wa Nishati, Dkt. Merdad Kalemani, amewataka wakandarasi wote nchini wanaotekeleza mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA III), kuhakikisha wanaweka umeme katika nyumba zote zikiwamo za tembe huku akipiga marufuku kurukwa.

Ameyasema hayo wakati akiwasha umeme katika vijiji vya Lukungu, Nyakaboja na Bukabile vilivyoko Wilaya ya Busega, mkoani Simiyu,

Amesema kuwa wamekuwa wakipata taarifa za wakandarasi waliopewa kazi ya kutekeleza mradi huo kuwa wamekuwa wakiziruka nyumba hizo kwa madai hazifai kupata huduma hiyo.

Aidha, amewataka wakandarasi hao kuhakikisha wanapeleka umeme katika kila kijiji na kila kitongoji ili wananchi waweze kuondokana na adha kubwa wanayokumbana nayo ya kukosa nishati ya umeme.

“Nimepata taarifa kuwa wananchi wenye nyumba za tembe wanarukwa, maagizo yangu ni marufuku kuruka nyumba ya tembe, tena nyumba hizo zipewe kipaumbele cha kwanza kupata umeme na hakuna kuruka kijiji, kitongoji au nyumba yoyote,” amesema Kalemani.

Hata hivyo, ameongeza kuwa Serikali haitaongeza muda, siku wala saa kwa mkandarasi yeyote atakayeshindwa kutekeleza mradi huo kwa muda muafaka waliopewa na Tanesco.

 

Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Agosti 19, 2018
Habari Picha: Spika Job Ndugai amjulia hali Dkt. Kigwangallah