Serikali imekemea vikali matukio ya vitendo vya ukatili wa kijinsia vinavyofanyika katika baadhi ya vyuo vya elimu ya juu nchini hatua ambayo inakuja ikiwa tayari kuna uwepo wa taarifa mbalimbali ambazo zimekuwa zikiripotiwa juu ya rushwa ya ngono.

Karipio hilo limetolewa jijini Dodoma na Katibu mkuu wizara ya afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto anayeshughulikia maendeleo ya jamii Dkt. John Jingu wakati akifungua kikao cha wakuu wa vyuo vya elimu ya juu kinachohusu namna ya kupambana na ukatili wa kijinsia katika maeneo ya vyuo vya elimu ya juu.

Amesema tatizo la ukatili wa kijinsia limekuwa likishamiri katika vyuo vya elimu ya juu kwani inaripotiwa kuwa wahadhiri wengi wamekuwa wakitumia madaraka yao vibaya kwa kuwalazimisha wanafunzi kufanya nao ngono ili waweze kuwasaidia kufaulu mitihani.

“Sio tu wanafunzi pekee wanaokumbana na vitendo hivyo hata wafanyakazi wanaofanya kazi katika vyuo vya elimu ya juu baadhi yao wanakutana na vitendo vya ukatili wa kijinsia sasa nguvu ya ziada inahitajika katika kupambana na vitendo kama hivi vyuoni,” amefafanua Dkt. Jingu.

Viwanja 208 vya ndege nchini vyapigwa ‘stop’

Ameongeza kuwa katika kuhakikisha wanapambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia Serikali na wadau wanatekeleza mpango mkakati wa kitaifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto ili kuhakikisha vitendo hivyo vinatokomezwa kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2030 nchini.

Dkt. Jingu pia amewataka wakuu hao wa vyuo kuhakikisha wanatoa elimu na maelekezo ili kujenga uelewa wa kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia hasa kwa wanafunzi wa kike kwa kwa ajili ya kuepuka matakwa ya wahadhiri wanaotumia hila kuendekeza vitendo vya ngono vyuoni.

Hata hivyo amewasisitiza wakuu wa vyuo kuhakikisha wanatekeleza agizo la waziri Ummy Mwalimu kuhusu kuanzisha madawati ya jinsia katika vyuoni ili kuwezesha kuondokana na vitendo vya kikatili na kujenga mazingira salama.

Magufuli aagiza vijana 800 wa JKT kuajiriwa

Awali mkuu wa uelimishaji kutoka Taasisi ya kupambana na kutokomeza rushwa (TAKUKURU), Asseri Mandari amesema wamejipanga vyema kupambana na tatizo hilo kwa kuanzisha Kampeni ya “vunja ukimya ondoa rushwa ya ngono” itakayosaidia kuondoa vitendo vya ukatili wa kijinsia hasa rushwa ya ngono.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa taasisi ya taaluma za jinsia toka chuo kikuu cha Dar es salaam Dkt. Lulu Mahai amesema vyuo vya elimu ya juu vinawajibu wa kutoa elimu kuhusu kupambana na vitendo vya kikatili kwa wanafunzi na wafanyakazi.

Amesema wanaamini baada ya kikao hicho watarudi na kuanzisha madawati ya kijinsia zikiwemo kamati mbalimbali ambazo zitakazosaidia kupambana na matukio ya ukatili wa kijinsia katika taasisi na
vyuo nchini.

Video: Siku 7 za roho juu usajili laini za simu, Hali ngumu zaidi sakata la ofisa LHRC
Hukumu yatolewa mauaji ya khashoggi , Majina ya wauaji yafichwa