Naibu Katibu Mkuu Afya, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Dkt. Dorothy Gwajima amewagiza waratibu wa timu za usimamizi huduma za afya Mikoa (RHMT) na Halmashauri (CHMT) nchini kuhakikisha, wameimarisha mifumo ya uwajibikaji ili kuleta mabadiliko katika sekta ya afya nchini.

Ameyasema hayo alipokuwa kwenye mwendelezo wa ziara zake za kikazi kwa lengo la kukagua uwajibikaji wa timu hizi kwa Mkoa wa Dodoma katika kituo cha afya cha Bahi kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Bahi Jijini Dodoma.

Amesema kuwa zoezi la kuwapima uwajibikaji limeanzia Mkoani Dodoma likiwa ni endelevu ambapo ndani ya siku 90 litakuwa limekamilika nchi nzima ambapo wale wote wasiopenda kubadilika watapangiwa majukumu mengine wanayoyamudu.

“Hakuna haja ya kila siku semina, warsha, mikutano halafu ukienda vituoni, mambo ya kawaida kabisa unakuta hayako vizuri wala takwimu hakuna na hakuna maelezo yoyote yenye mashiko kwa nini hali imekuwa hivyo ilivyo” Amesema Dkt. Gwajima.

Aidha, amesema kuwa pamoja na kazi nzuri zinazofanywa katika baadhi ya maeneo, yapo masuala ya msingi ambayo, yanahitaji kusimamiwa vizuri zaidi na hayahitaji chochote cha ziada zaidi ya uwajibikaji imara wa viongozi waliopewa dhamana.

Dkt. Gwajima amesema, Serikali haitavumilia kuwa na waratibu ambao, hawaleti msukumo katika kuleta mabadiliko ya uwajibikaji na badala yake wamebaki kusafiri na kuhudhuria semina, warsha na mikutano ambayo haileti tija katika maeneo yao ya kazi.

Katika hatua nyingine, Dkt. Gwajima ameawaagiza waratibu kufanya usimamizi na ufuatiliaji kwa weledi mkubwa ambapo kila mmoja atatakiwa kuonyesha ameona nini na mpango kazi ni upi na umefanikisha ufumbuzi wa changamoto ngapi, kama umekwama je, amechukua hatua gani za kuomba msaada.

Kuhusu ushirikishwaji wa wadau, amezielekeza timu hizo kuwa na Kamati za Afya za Vituo na Bodi za Afya ambazo, ni wawakilishi wa wananchi ziwezeshwe ili, kuimarisha kiungo kati ya kituo na wananchi wanaowakilishwa na Kamati hizo.

Hata hivyo, Dkt. Gwajima ametoa wito kwa timu za afya nchini kujifunza toka timu za Dodoma ambao, kwa kutumia fursa ya kuwa karibu na Wizara wameona kwa vitendo nini kinatakiwa ili, nao waanze mara moja kuimarisha mifumo na kuanza mbio za mabadiliko kabla zoezi la tathmini ya Wizara halijawafikia hivyo RHMT na CHMT zinahitajika kuwa imara ili, kuchochea huduma bora katika vituo vya tiba.

 

CCM Njombe yatoa ufafanuzi zoezi la uhakiki wa mali za chama
Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Machi 18, 2019