Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Bashiru Ally amewazungumzia wabunge vijana wa chama hicho, Nape Nnauye (Mtama) na Hussein Bashe (Nzega Mjini), akieleza kuwa ni vijana watukutu na wadadisi wanaotakiwa kupikwa na kusimamiwa.

Akizungumza katika mahojiano na Tido Mhando kupitia ZBC2, Dkt. Bashiru amesema kuwa wabunge hao ni zao la Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) ambao walipikwa baada ya mfumo wa kuwandaa viongozi kufa.

“Sasa Umoja wa Vijana ambao ulikuwa ndio tanuru la vijana, likakosa hiyo faida ya vijana kuandaliwa. Sasa akina Bashe na Nape wametokea Umoja wa Vijana kipindi ambacho maandalizi yao yalikuwa yanasuasua, kipindi ambacho Umoja wa Vijana ukageuzwa kuwa chombo cha kujipima umaarufu wao, hasa wagombea Urais,” alisema Dkt. Bashiru.

“Kwa bahati mbaya chama kikawa mbali na vijana wale, na bahati mbaya vijana ni watukutu, wakati wote akili inachemka. Ndivyo Bashe na Nape walivyopatikana, walitokea Umoja wa Vijana, wakaaminiwa, wakapewa nafasi za uongozi wakaenda wakawa Wabunge kwahiyo ule udadisi wao unaonekana una usumbufu fulani,” aliongeza.

Alimtolea mfano Nape ambaye alikuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho hususan wakati wa Awamu ya Nne, alisema alifanya kazi kubwa lakini anahitaji kupikwa zaidi, kusikilizwa, kuaminiwa na kusimamiwa.

Nape na Bashe wamekuwa wakionesha misimamo mikali Bungeni wakiwahoji Mawaziri kuhusu masuala mbalimbali.

Vurugu zazuka kanisani baada ya Bwana Harusi kudaiwa ni mume wa mtu
Waokoaji wapata mtihani kwenye vijiji vilivyokumbwa na Kimbunga