Naibu Waziri wa Fedha na Mipango. Dkt. Ashatu Kijaji, ameiagiza Wakala wa majengo Tanzania-TBA, kutekeleza kwa wakati mradi wa ujenzi wa Ofisi ya Halmashauri ya Mji wa Kasulu Mkoani Kigoma ili kuiepusha Serikali kutumia fedha nyingi kutokana na kuongezeka kwa gharama za miradi husika kunakotokana na ucheleweshwaji huo.

Ametoa agizo hilo baada ya kukagua maendelelo ya ujenzi wa Ofisi mpya za Halmashauri ya Mji wa Kasulu zinazojengwa na Serikali kwa zaidi ya shilingi bilioni 2.5 na kutaarifiwa kuwa TBA, wamechelewa kuanza ujenzi huo kwa zaidi ya miezi 12 wakati fedha zilikwisha tolewa na Serikali.

Ameitaka TBA kujipanga kukamilisha miradi inayopewa na Serikali kwa wakati kwa kuongeza idadi ya wataalam wanaoweza kusimamia miradi mingi inayotekelezwa na wakala huo.

“Pesa zipo, Serikali haiwezi kuanza kutekeleza mradi wowote kama hakuna pesa, ni jukumu lenu kama TBA kuhakikisha mnawezesha mradi huu ukamilike kwa wakati ili tupate thamani halisi ya fedha za mradi,” amesema Dkt. Kijaji

Aidha, Dkt. Kijaji ametoa wito kwa wakazi wa Mji wa Kasulu na Kigoma kwa ujumla kuchangamkia fursa za ujenzi wa miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali katika maeneo yao kwani lengo la Serikali kujenga miradi hiyo ni kuwawezesha pia wananchi kiuchumi.

Hata hivyo, hatua hiyo inafuatia taarifa iliyotolewa na Mhandisi wa ujenzi wa Jengo hilo la Ofisi ya Halmashauri ya Mji wa Kasulu, Abubakari Basuka, kwamba miongoni mwa changamoto inayoukabili mradi huo ni ukosefu wa mafundi mchundo na vibarua ambapo imeelezwa kuwa vijana wengi katika eneo la mradi hawajitumi kufanyakazi.

 

Video: Vurugu zatawala uchaguzi Arusha, Kubenea afunguka kuhamia CCM
Lowassa afunguka madai ya ‘kuwatanguliza watu CCM’

Comments

comments