Siku kadhaa baada ya akaunti ya Twitter ya Katibu Mkuu wa Chadema, Dkt. Wilbroad Slaa kutekwa na mdukuzi walioanza kuandika kile anachotaka, Dkt. Slaa amejitokeza na kumuonya mtu huyo anayetumia jina lake.

‘Yericko Nyerere’, ni jina analotumia mdukuzi wa akaunti ya Dkt. Slaa na amekuwa akiandika taarifa nyingi zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zikionesha kuwa zimetoka moja kwa moja kwa mwanasiasa huyo.

Sehemu kubwa ya majibu ya Yericko yamelenga katika tetesi zinazodai kuwa Dkt. Slaa amejitoa Chadema baada ya kutokubaliana na uamuzi wa chama chake kumkaribisha Edward Lowassa kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho.

Hatimaye, Dk. Slaa alijitokeza kupitia akaunti yake kama mtumiaji aliyethibitishwa ya Jamii Forum (Verified user) baada ya kukaribishwa na waendeshaji rasmi wa mijadala katika mtandao huo ili kufunga mjadala uliokuwa unaendelea. Slaa alimjibu mtu huyo aliyekuwa ameeneza habari kuwa atashiriki katika vikao vya Kamati Kuu ya Chadema hivi karibuni pamoja na vikao vingine vya Secretariat.

Pia alitoa onyo kwa mtu yeyote anaetumia jina lake kutoa taarifa na kwamba endapo yeye atahitaji kutoa taarifa yoyote ile ataita vyombo vya habari au atatumia njia rasmi na si vinginevyo.

“Sipendi Siasa ya unafiki sipendi. Nimenyamaza lakini naona mnazidi kunichokoza. Ni afadhali mngelikaa kimya kama nilivyonyamaza mimi. Uwongo wowote na upotoshwaji wowote sitauvumilia. Nitaukanusha hapo hapo. Hata kama una lengo lako ambalo silifahamu naomba sana usitumie jina langu. Nimefundishwa uwongo ni dhambi siko tayari kushiriki dhambi hiyo.

“Sina kikao chochote cha Secretariat sina mpango wowote ninaopanga kuwasilisha popote. Naomba watanzania wapuuze propaganda zote zinazofanyika kwa jina langu.

“Ningehitaji kutuma taarifa yoyote kwa umma ningeliita Press Conference Mwenyewe au ningelitumia utaratibu wowote uliouliozoeleka. Naomba kutoa onyo kwa mtu yeyote awaye, matumizi ya jina la Dr Slaa yakome.

Hivi karibuni, Dkt. Slaa alikanusha taarifa kuwa amefungiwa ndani ya nyumba na mkewe ambaye pia alimshawishi kutounga mkono uamuzi wa Chadema kumkaribisha Lowassa.

Makongoro Mahanga: CCM Walinionya Kuhusu Lowassa
Nape ‘Atiririka’ Baada Ya Kushikiliwa Na Takukuru Kwa Tuhuma Za Rushwa