Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Wilbroad Slaa atajiwa kujiunga na makamanda wa chama hicho katika kampeni za uchaguzi mkuu, zitakazoanza Agosti 22 mwaka huu.

Hayo yameelezwa na mbunge wa jimbo Ubungo anaemaliza muda wake na anaegombea katika jimbo jipya la Kibamba, John Mnyika, wakati akizumza na viongozi wa Chadema wa matawi ya kata ya Goba, wiki iliyopita.

“Dk. Slaa yupo mapumzikoni na jana nilizungumza naye kwa kirefu na aliniambia bado anapumzika, lakini atakuja kushiriki kampeni jimbo la Kibamba ambalo mimi nagombea ubunge,” Mnyika anakaririwa.

Tamko hilo la Mnyika linakuja wakati ambapo wanachama wengi wa chama hicho wanatamani kuiona sura ya Dk. Slaa na kusikia sauti yake katika majukwaa ya chama hicho na Ukawa kwa ujumla ili kuongeza nguvu safari yao ya kutaka kushika dola.

Hata hivyo, bado haijafahamika kama Dk. Slaa atajiunga rasmi na kampeni za Ukawa kwa ujumla au atampigia debe John Mnyika pekee katika uzinduzi wa kampeni ya jimbo la Kibamba.

Dk. Slaa yuko katika mapumziko ya kipindi kisichojulikana kutokana na kutokubaliana na maamuzi ya chama chake kumkaribisha Edward Lowassa na kumpa nafasi ya kugombea nafasi ya urais kupitia chama hicho.

Katika hatua nyingine, leo mchana maelfu ya wafuasi wa vyama vinavyounda Ukawa wamemsindikiza mgombea urais, Edward Lowassa kuchukua fomu katika ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), jijini Dar Es Salaam. Barabara kadhaa za jiji hilo zimelazimika kufungwa huku makundi mbalimbali ya vijana yakionekana yakifanya mbwembwe za kila aina.

Wananchi waliokuwa katika eneo la Posta wameshuhudia vijana waliomsindikiza Lowassa wakionesha mbwembwe za mchezo wa Karate, ufundi wa kuendesha pikipiki (bodaboda), kucheza muziki kwenye magari maalum ya wazi, kuimba nyimbo mbalimbali zinazomtaja Lowassa na mengineyo.

Tenga, Malinzi Waula CAF
TWIGA STARS YAENDELEA KUJIFUA ZANZIBAR