Ange Di Huon maarufu kama DJ Arafat, msanii maarufu kutoka Ivory Coast amefariki dunia leo, Agosti 12, 2019 baada ya kupata ajali akiwa anaendesha pikipiki usiku wa kuamkia leo.

Mfalme huyo wa ‘coupe decale’ amepoteza maisha akiwa anapatiwa matibabu hospitalini mjini Abidjan, kutokana na majeraha aliyoyapata baada ya pikipiki aliyokuwa anaiendesha kugongwa na gari, kwa mujibu wa Waziri wa Utamaduni wa nchi hiyo, Maurice Bandaman.

Waziri Bandaman amesema pikipiki aliyokuwa anaiendesha Dj Arafat iligongwa na gari lililokuwa linaendeshwa na mtangazaji maarufu wa redio nchini humo.

Daktari wa hospitali aliyokuwa anapatiwa matibabu amewaambia waandishi wa habari kwa masharti ya kutotajwa jina kuwa msanii huyo alikuwa amepasuka sehemu ya fuvu.

“Alilazwa kwenye chumba cha dharura akiwa kwenye hali mbaya. Alikuwa na jeraha/mpasuko kwenye eneo la fuvu. Tulijaribu kumsaidia na kuokoa maisha yake lakini tulishindwa” daktari aliwaambia waandishi wa habari.

Taarifa za kifo cha Dj Arafat zilitolewa na Waziri wa Utamaduni, Bandaman.

“Niko hospitalini muda huu alipokuwa amelazwa DJ Arafat na naweza kuthibitisha kuwa amefariki dunia,” Bandaman anakaririwa na Jeune Afrique.

Wimbo wa mwisho alioutoa ni ‘Moto moto’ ambao hadi sasa umetazamwa zaidi ya mara milioni 4.4 kwenye YouTube ndani ya miezi mitatu.

Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Agosti 13, 2019
Wizara ya Ujenzi yapeleka watumishi 44 katika miradi ya miundombinu