Mabingwa wa soka Tanzania bara Wekundu wa Msimbazi Simba wapo kwenye harakati za kumshawishi mshambuliaji wa pembeni kutoka DR Congo Deo Kanda, ili asaini mkataba wa kuendelea kubaki nchini.

Simba ipo kwenye mpango wa kujihakikishia kutwaa ubingwa wa ligi kuu kwa msimu wa tatu mfululizo, huku ikianza mikakati ya kujenga kikosi imara ambacho kitatoa ushindani kwenye michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika msimu ujao.

Kanda ni mchezaji mwenye uzoefu mkubwa wa michuano hiyo, alitua Simba kwa mkopo wa mwaka mmoja akitokea TP Mazembe, ambao unamalizika mwezi Juni.

Mkongomani huyo bado hajatoa maamuzi yake kama atabakia Simba SC ama atarudi kuongeza mkataba mpya TP Mazembe ambayo inammiliki nyota huyo mpaka Juni mwaka huu mkataba wake utakapomalizika.

Kutimuliwa kwa kocha Mihayo Kazembe kunaweza kumshawishi Kanda kusaini mkataba mwingine na mabingwa hao wa DRC.

Inaelezwa Kanda hakuwa na maelewano mazuri na Kazembe na ndio sababu iliyofanya nyota huyo alazimishe kuondoka kwa mkopo klabuni hapo mwishoni mwa msimu uliopita.

Baada ya kutolewa hatua ya robo fainali michuano ya ligi ya mabingwa, uongozi wa TP Mazembe ulimsimamisha Kazembe na inaelezwa hatarejea kuendelea kuinoa timu hiyo.

Hata hivyo pamoja na mazingira hayo, Simba ina nafasi nzuri ya kumnasa Kanda kwa kuwa ndio wapo nae mpaka sasa. Kanda amefunga mabao sita kwenye ligi kuu Tanzania bara.

Shinyanga: Soko lanusurika kuteketea kisa Sigara
Waziri Mkuu kuongoza mamia kumuenzi Mengi