Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe, Ally Kasinge ameagiza kila mwananchi kuhakikisha anashirikiana na serikali kudhibiti mimba kwa wanafunzi katika wilaya hiyo kutokana na takwimu ya wanafunzi wanaopata ujauzito mashuleni kuendelea kuongezeka.

Ametoa agizo hilo katika kikao cha tathmini ya elimu kilichofanyika wilayani hapo mara baada ya kusomewa takwimu za idara ya elimu zilizobainisha wanafunzi 22 kukatishwa masomo mwaka jana huku kuanzia Januari 2019 hadi sasa wanafunzi 6 wakikatishwa masomo yao.

“Uwe kiongozi, uwe mwananchi,uwe mchungaji, uwe mwalimu, uwe askari lazima tuhakikishe tunafanya kazi ya kudhibiti mimba ya wanafunzi wa kike katika wilaya yetu, kila mtu atimize wajibu wake na kwenye hili hatutamuacha mtu endapo haya yakiendelea, takwimu hizi mmeziona,”amesema Kasinge

Kwa mujibu wa takwimu za idara ya elimu zilizotolewa na Maofisa Elimu Sekondari na Msingi imebainisha kuwa wanafunzi 22 walikatishwa masomo mwaka jana huku kuanzia Januari 2019 hadi sasa wanafunzi 6 wamekatishwa masomo huku pia kuhusu utoro ikielezwa wanafunzi 166 hawakuripoti shule mwaka 2018 na wanafunzi 187 kwa 2019 jambo ambalo linaisukuma serikali kuchukua hatua.

Nao baadhi ya wadau wa elimu ambao wameshiriki katika kikao cha cha tathmini ya elimu wamekiri wilaya hiyo kukabiliwa na changamoto kubwa ya wazazi kushinikiza watoto wao kujiferisha mitihani na kuhitaji hatua kali kuchukuliwa dhidi yao.

Hata hivyo, halmashauri ya wilaya ya Wanging’ombe ni miongoni mwa halmashauri mbili za mwisho kitaaluma kati ya 6 za mkoa wa Njombe 2019.

Msanii Bright, Mafuriko yamenifanya nivae nguo moja
Waziri Mkuu atinga suti ya sketi